Lissu aoneshwa gari lake, ataka waliohusika washughulikiwe

Mwonekano wa gari la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana mkoani Dodoma Septemba 7, 2017. Picha na maktaba

Muktasari:

Lissu alikutana na mkasa huo mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari hilo akijiandaa kushuka nyumbani kwake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge, ambapo watu wasiojulikana walimshambulia kwa risasi.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kulilinda gari lake baada ya shambulio la risasi kutoka kwa watu wasiojulikana.


Lissu (55) alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari hilo akijiandaa kushuka nyumbani kwake, Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.


Akizungumza Dodoma leo Jumanne Mei 9, 2023 baada ya kuliona gari hilo kwa mara ya kwanza amesema alifanya mawasiliano na uongozi wa Polisi mkoa huo pamoja na maafisa wake ndipo walipomruhusu kuliona.


“Hii gari imekuwa chini ya Polisi kwa muda wote huu na mimi binafsi nilikuwa sijawahi kuliona kabisa, nilikuwa nasikia tu kwamba nilipigwa risasi nyingi, leo wameniwezesha nimeona ina matundu 30 ya risasi na imenipa shida sana nashukuru kwa kulilinda gari hii,” amesema.


Ameshangaa kuona risasi zote kuelekezwa kwenye mwili wa mtu mmoja na kwamba baada ya kuliona gari hilo atafanya mawasiliano na Jeshi hilo ili aende kulichukua.

Soma zaidi: Undani wa Tundu Lissu kupigwa risasi
“Wanikabidhi na maisha mengine yaendelee, nafikiri kwa sababu kumekuwa na maneno maneno mengi kwamba Polisi gari wanaikatalia, naomba niseme hapa wazi polisi hawajawahi kuwa na wazo la kunikatalia kuchukua gari yangu,” amesema.


Ameeleza kilichokuwa kinatokea alipokuwa akienda kulitazama gari hilo, watendaji wa jeshi hilo walikuwa na shughuli nyingi.
 “Ni Jamhuri na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ikiwemo jeshi la Polisi wanamaamuzi. Kielelezo (gari) wamekaa nacho zaidi ya miaka sita, kama ni picha wamepiga na kuangalia risasi ilipita wapi watakuwa wamefanya,” amesema


Hata hivyo, Lissu amelitaka Jeshi la Polisi kuwatafuta waliofanya tukio hilo washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.


“Mimi ningependa huyo aliyepiga hizo risasi zote hizo atafutwe na ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria,” amesema