Ole Sendeka: Vijana gombeeni nafasi za CCM mwakani

Wednesday September 29 2021
vijanapic
By Joseph Lyimo

Mirerani. Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka amewataka vijana wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za chama hicho mwaka 2022.

Uchaguzi mkuu wa CCM kugombea nafasi kuanzia ngazi ya tawi, kata, wilaya, mkoa hadi Taifa unatarajia kufanyika mwaka 2022.

Ole Sendeka ameyasema hayo leo Septemba 29, katika mji mdogo wa Mirerani, kwenye kikao cha baraza la jumuiya ya umoja wa vijana wa chama hicho (UVCCM) wa Wilaya ya Simanjiro.


Amesema vijana wa CCM wanapaswa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali pindi muda wa uchaguzi wa chama hicho ukiwadia kwani ni haki yao.

"Ninasema hili kwa vijana na nitasema pia kwa jumuiya nyingine za chama za wazazi na wanawake, kwani ni haki yao ya msingi katika kugombea uongozi kwenye chama," amesema Ole Sendeka.

Advertisement

Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Simanjiro, Thomas Mollel amesema vijana ndiyo jeuri ya chama hivyo anatarajia wengi wao watajitokeza kugombea nafasi mbalimbali mwakani wakijaliwa uzima.

Mollel amesema vijana wa Simanjiro wana ari kubwa na matarajio ya kugombea uongozi wa ngazi ya chama kwani wamepikwa na kuiva tayari kukitumikia chama hicho

"Pamoja na hayo ninawapongeza vijana wote kwa kumuunga mkono kijana mwenzetu wa Simanjiro, Mosses Komba hadi akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM wa mkoa wa Manyara," amesema Mollel.

Mbunge wa Vijana Taifa kupitia mkoa wa Manyara, Asia Halamga amewashukuru wajumbe wa wilaya hiyo waliofanikisha ushindi wake mwaka jana kwa kumpigia kura nyingi za ushindi mjini Babati.

"Uchaguzi ulishapita hivi sasa ni muda wa kuwatumikia vijana wenzangu, naamini umoja wetu ni ushindi wetu hivyo tutauendeleza," amesema Halamga.


Advertisement