Onyesho la askari wanawake kuwalinda viongozi laacha watu midomo wazi

Muktasari:
- Onyesho la askari wanawake wanavyoweza kuwalinda viongozi wanapofanyiwa uvamizi na maadui limekuwa kivutio wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, katika uwanja wa Samora, Mjini Iringa.
Iringa. Onyesho la wanawake askari wa Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limegeuka kivutio hasa walipoanza kupiga risasi wakati wakijaribu kumuokoa kiongozi aliyevamiwa na adui.
Askari hao walionyesha umma umahiri wao katika kupambana na maadui leo Machi 4, hasa viongozi wanapofika kwa ajili ya kuhutubia au ukaguzi wa shughuli za maendeleo.
Awali, lilifika gari la kiongozi na alitefunguliwa mlango lakini wakati akiendelea kusalimia wananchi, walitokea wavamizi amboa walipiga risasi kisha askari hao kuonyesha namna wanavyoweza kumuokoa askari.
Baadae walianza kurushiana risasi huku, wakiwataka wananchi wasiwe na wasiwasi kwa milio inayosikika kwa sababu ilikuwa ni onyesho.
Pamoja na onyesho hilo, wanawake walipita na vyombo mbalimbali vya moto kama bodaboda, bajaj, mabasi, gari za polisi na magari makubwa ya kubeba mchanga.
Mkuu wa Usalama Barabarani, Mkoani Iringa (RTO) Mosi Ndozero akiwa kiongozi wa kikosi hicho cha wanawake alisema wanawake wanao uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali kwenye jamii kama ilivyo kwa wanaume.
Akizungumza katika onyesho, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amewataka wanawake wa mkoa huo kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku wakipambana na ukatili wa kijinsia ikiwamo kuwalinda watoto.
Amesema mafanikio ya mwanamke yanahitaji weledi na kujituma na kwamba, wakifanya kazi wa bidii wataendelea kuchangia uchumi wa mkoa huo na Taifa.
“Suala la lishe muhimu sana, tuendelea kupambana na udumavu,” alisema.
Kwa upande wao baadhi ya wanawake, walisema bado jamii inatakiwa kuendelea kupewa elimu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia.