Onyo kwa wanaonunua miwani holela mitaani

Mkurugenzi wa kampuni ya Swift Groups Of Companies, Mohammed Hussein Dewji akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya upimaji macho kwa wanafunzi wa shule ya msingi nchi nzima.

Muktasari:

  • Mtaalamu abainisha miwani inaweza kupunguza uono, kuleta magonjwa ya macho na shida nyingine.

Dar es Salaam. Mtaalamu wa macho ameonya tabia ya watu kununua miwani holela na kuivaa, akisema inaweza kupunguza uwezo wa kuona wa mvaaji.

 Badala yake, ameshauri kabla ya kuvaa miwani, mtu apimwe na wataalamu ili kujua aina ya miwani anayopaswa kuvaa.

Amesema miwani huwa na namba ambayo inapaswa kulingana na nguvu ya macho ya mvaaji.

Hii inawahusu zaidi wale wanaonunua miwani mitaani, hususani ya kuzuia mionzi ya jua na kuvaa bila kufuata utaratibu.

Ushauri huo umetolewa jana Aprili 15, 2024 wakati wa hafla ya uzinduzi wa upimaji macho na kugawa miwani bure kwa wanafunzi wa shule za msingi Tanzania uliofanyika katika Shule ya Msingi Kilamba, iliyopo Mbagala, mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, chini ya udhamini wa kampuni ya Swift Group of Companies, Maria Michael ambaye ni mtaalamu wa macho amesema miwani pia inapaswa kuhifadhiwa katika hali ya usafi na si vumbi.

“Miwani inaweza kupunguza uono, kuleta magonjwa ya macho na shida nyingine. Tunashauri jamii ni vyema kumuona mtaalamu, ili tupewe namba ya lensi inayoendana na nguvu ya macho kwani bila kufanya hivyo uoni huweza kupungua pasipo kujua,” amesema.

Ili kujua nguvu ya macho na aina ya miwani anayopaswa kuvaa mtu, amesema vipimo maalumu hufanyika kwenye macho ya mhusika ambavyo hutumika kutengeneza lensi ambayo akiivaa haitamletea shida.

Hata hivyo, imezoeleka mtaani kuwaona wauzaji wa miwani wakiitembeza na kuuza.

Miwani hiyo imekuwa ikipigwa vumbi na jua kali, lakini watu wamekuwa wakinunua kwa kuangalia mwonekano wake bila kujali athari zinazoweza kujitokeza baada ya kuivaa.

Mkurugenzi wa Swift Group of Companies, Mohammed Dewji amesema ameamua kupeleka mradi wa kupima macho kwa watoto shuleni kubaini matatizo yao mapema.

“Gharama ya mradi huu ni Sh170 milioni, mpango wetu ni kuanza na shule hii yenye watoto 3,085. Tunatarajia kupima wanafunzi 100 kila siku na itatuchukua zaidi ya mwezi mmoja kukamilisha kazi,” amesema.

Dewji kupitia taarifa kwa vyombo vya habari amesema watakapomaliza shule hiyo watakwenda nyingine ndani ya Jiji la Dar es Salaam kabla ya kwenda mikoa yote nchini.

Amesema wazo hilo alilipata alipokwenda Afrika Kusini ambako mmoja wa jamaa zake alimuambia kupitia sensa ya aina hiyo waliyoifanya nchi nzima walibaini asilimia 30 ya watoto wana shida ya macho.

“Watoto wanapata shida na kushindwa kusoma, wazazi na walimu wanadhani wanafunzi hawaelewi kumbe wana shida ya macho, niliona asilimia hizi ni nyingi nikaona na mimi nijaribu kufanya nchini, kwani wanopokuwa darasani maisha yao yatakuwa bora zaidi,” amesema Dewji.

Huduma ya upimaji wa macho katika shule za msingi nchini inafanyika kwa kutumia kliniki inayotembea (Mobile Clinic).

Twahil Kamona, diwani wa Charambe amesema viongozi na wazazi wako tayari kuhakikisha upimaji unafanikiwa.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kilamba, Leah Masaba amesema wakati mwingine wamekuwa wakisema watoto wanafeli bila kujua chanzo huenda shida ikawa ni ya macho.

“Wakipimwa tunaweza kujua shida ni nini, tunashukuru kwa msaada huu, kwani utawasaidia watoto wote wa shule kuanzia darasa la awali hadi la saba,” amesema Masaba.

Amour Amri, kiongozi wa wanafunzi shuleni hapo amesema huduma hiyo itawasaidia kutambua hali yao ya afya ya macho.

“Tunajifunza tusidharau kitu, mimi macho yaalikuwa yananiuma nikapuuzia, leo wamenipima wamegundua nina tatizo la macho,” amesema Amri.