Panya road wadaiwa kuvamia nyumba 24 Dar, wajeruhi wanne

Muktasari:

  • Maisha ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam yameendelea kukumbwa na wasiwasi, baada ya vikundi vya uhalifu maarufu Panya Road kurudi tena na kuvamia nyumba 24 za wapangaji wa mtaa wa Kabaga Kinyerezi kisha kuwajeruhi nakupora mali zao.

Dar es Salaam. Maisha ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam yameendelea kukumbwa na wasiwasi, baada ya vikundi vya uhalifu maarufu Panya Road kurudi tena na kuvamia nyumba 24 za wapangaji wa mtaa wa Kabaga Kinyerezi kisha kuwajeruhi nakupora mali zao.

Kwa mujibu wa wananchi wa Kabaga wameeleza tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana Jumanne Septemba 06, 2022 saa 8 usiku katika maeneo hayo ambapo raia wanne wamejeruhiwa na kwa sasa wapo hospitali ya Amana wakipatiwa matibabu.

Hata hivyo, alipotafutwa Kaimu Kamanda wa Kanda hiyo, Wiliam Mkonda kujua uhalisia wake, amekiri kutokea kwa tukio hilo huku akieleza "Taarifa za tukio hilo nilisha zielezea toka jana."

Matukio hayo yanarudi ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, licha ya Serikali kupitia jeshi la Polisi kanda Maalumu, kutangaza vita dhidi ya vikundi vinavyotekeleza vitendo hivyo vinavyoacha hasara ya kiuchumi kwa jamii hususan wahanga wa matukio hayo.

Wakizungumza leo Jumatano Septemba 07, 2022, wahanga wa tukio hilo, wamesema hawawezi kusahau maishani mwao kwani wamefanyiwa unyama na hata walinzi (Sungusungu) waliokuwa wanawategemea waliwakimbia, kuwacha wakisurubiwa.

Zahoro Juma, aliyejeruhiwa na kuibiwa pikipiki mpya aina ya Boxer 125 amesimulia wakati wanakuja kuvamia ‘Apartment’ yao yenye nyumba 14 walikuwa vijana zaidi ya 30 huku wengine wakiwasubiri nje wakiwa kwenye Bodaboda.

"Wakiwa wanapiga baruti, walianza kuvamia nyumba moja hadi nyingine kuvunja milango kujeruhi na kuchukua wanachokitaka, na watu waliokuwa wanapiga kelele kama akina Mama wamejeruhiwa kwa kupigwa mapanga maeneo mbalimbali ya mili yao," amesema

Jakson Joseph aliyejeruhiwa kwa kupigwa mapanga kichwani mara tatu na miguuni amesema vijana hao walikuwa wadogo na hatari kwa kuzingatia walivyomshambulia wakati anatoka ndani kwake kwa lengo la kutaka kwenda kumsaidia jirani yake.

"Vijana ni wadogo lakini ni hatari wanaua nisingekimbia sijuhi nini kingeendelea, Serikali inapaswa kuwa makini watu tunawasiwasi hatuna amani watusaidie kwenye masuala ya ulinzi," amesema

Mwenyekiti wa mtaa huo, Hashimu Gulana amesikitishwa na tukio hilo huku akiwalaumu wananchi wa mtaa huo kushindwa kupigiana simu kuwadhibiti vijana hao waliodumu kwenye eneo hilo kwa saa mbili wakitekeleza vitendo hivyo.

"Baada ya tukio, Polisi walikuja, lakini naomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa sababu hata tukio linatokea walikuwa wanachungulia madirishani badala wapigiane simu kuwadhibiti vijana hao," amesema