Papa Francis amteua Padri Kibozi kuwa Askofu Msaidizi Dodoma

Askofu Msaidizi mteule wa Jimbo la Dodoma, Wilbroad Kibozi (katika) akiwa pamoja na  Monsinyori Pius Rutechura, gombera wa Seminari Kuu ya Kitaifa ya Familia Takatifu, Mwendakulima iliyopo Jimbo la Kahama mkoani Shinyanga na kulia ni Askofu Christopher Ndizeye wa Jimbo la Kaham

Muktasari:

  • Uteuzi huo umefanyika leo Jumatatu Februari 12, 2024. Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican, Padri Kibozi alisoma masomo yake ya falsafa katika Seminari Kuu ya Ntungamo iliyopo mkoani Kagera.

Dar es Salaam. Papa Francis amemteua Padri Wilbroad Kibozi kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dodoma.

Uteuzi huo umefanyika leo Jumatatu Februari 12, 2024 na kutangazwa kupitia taarifa iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na kusainiwa na Katibu Mkuu wake, Padri Charles Kitima.

Kabla ya uteuzi huo, Padri Kibozi alikuwa makamu Gombera, mlezi na mwalimu wa Seminari Kuu ya Kitaifa ya Familia Takatifu, Mwendakulima iliyopo Jimbo la Kahama mkoani Shinyanga.

Askofu huyo mteule alizaliwa Aprili 30, 1970 katika eneo la Lumuna, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.

Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican, Padri Kibozi alisoma masomo yake ya falsafa katika Seminari Kuu ya Ntungamo na masomo ya thiolojia katika Seminari Kuu ya Kipalapala, Jimbo Kuu Katoliki la Tabora.

“Baada ya kufanya shughuli za kichungaji kwa muda wa mwaka mmoja katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji huko Chalinze (Dodoma), aliendelea na masomo na kupata leseni na Shahada ya Udaktari wa taalimungu (thiolojia) katika Kitivo nchini Italia,” imeandika tovuti ya Vatican.

Vilevile, tovuti hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki duniani imesema alipewa daraja takatifu la upadri Julai 9, 2010 kwa ajili ya utumishi katika jimbo lake la Dodoma.


Nyadhifa alizowahi kushika

Padri Kibozi aliwahi kuwa paroko msaizidi wa Lumuma (2010-2012); Mkurugenzi wa Miito Jimbo Kuu la Dodoma (2012-2014) na Muungamishi katika Nyumba ya Malezi Livorno, Italia (2017-2019).

Pia amehudumu kama mkufunzi wa waseminari katika Chuo Kikuu cha Jordan, Morogoro (2019-2020) kabla ya kuwa makamu gombera katika Seminari Kuu ya Mwendakulima, Kahama.