Picha ilivyoibua umaarufu, kutwaa uhai wa Carter- 1

Muktasari:

Picha yenyewe ilipata umaarufu sana duniani hadi ikaitwa The Vulture and the Little Girl (Tai na Msichana Mdogo).

Picha yenyewe ilipata umaarufu sana duniani hadi ikaitwa The Vulture and the Little Girl (Tai na Msichana Mdogo).

Ilijizolea umaarufu mkubwa hata kushinda Tuzo maarufu ya 'Pulitzer ya upigaji picha bora duniani na ilikuwa maarufu zaidi duniani katika kipindi cha mwaka 1993 na 1994.

Aliyeipiga picha hiyo ni Kelvin Carter, mzaliwa wa Johannesburg, Afrika Kusini. Ilionekana kwa mara ya kwanza ilipochapishwa katika gazeti la Marekani la 'New York Times' toleo la Machi 26, 1993.

Maelezo yaliyochapishwa chini ya picha hiyo yanasomeka, "Msichana mdogo, aliyedhoofika kwa njaa, alianguka hivi majuzi kando ya njia kuelekea kituo cha kutoa msaada wa chakula huko Ayod. Karibu naye, tai akisubiri."

Ilionyesha hali ya kusikitisha iliyosababishwa na njaa kali nchini Sudan mwaka 1993. Lakini baadaye ikajulikana kuwa mtoto yule hakuwa msichana bali ni mvulana dhaifu aliyekumbwa na njaa. Mtoto huyo alijaribu kufikia kituo cha chakula cha Umoja wa Mataifa kilichokuwa umbali wa nusu maili huko Ayod, Sudan (sasa Sudan Kusini) wakati tai akimkaribia kwa lengo la kumla.

Ingawa ilishinda tuzo ya picha bora duniani, wengi waliichukulia ya kikatili kiasi kwamba mhariri wa gazeti la 'The Times', akizingatia hisia za wasomaji, alichapisha maandishi juu ya hatima ya mtoto huyo.

Aliandika: "Bwana Carter alisema alianza tena safari yake hadi kwenye kituo cha chakula na alimfukuza tai." Lakini gazeti 'The Guardian' la Uingereza lilikuwa na habari iliyosomeka kwamba Carter hakuingilia kati kumfukuza tai huyo.

Carter hakumsaidia mtoto huyo kwa sababu, liliandika gazeti hilo, ‘kulikuwa na maelfu kama (mtoto) huyo.

Likiandika kuhusu picha hiyo, 'The Times' liliandika hivi: "Kwa (gazeti) ‘The New York Times, picha iliyopigwa na Kevin Carter ya tai akiwa karibu na msichana mdogo nchini Sudan ambaye ameanguka kutokana na njaa, iligeuka kuwa ishara ya njaa."

Picha ilipoonekana kwa mara ya kwanza, iliambatana na habari ya njaa ambayo kwa mara nyingine ilitokana na ghasia za kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kusini mwa Sudan.

Katika picha hiyo mtoto anaonekana akiwa uchi, aliyedhoofika, mgonjwa na asiyeweza kutembea kutokana na kudhoofika huko. Pamoja na hayo yote, hakukuwa na mtu wa kumsaidia wala kumlinda. Hakuna mama, familia wala mtu wa kumzuia asishambuliwe na tai au kufa njaa na kuliwa kama mzoga.

Wasomaji wa gazeti lililochapisha picha hiyo walijikuta wakiwazia mateso mengi yaliyomfikisha mtoto huyo katika hali hiyo. Je, familia yake iliangamizwa na machafuko hayo? Aliachwa ajifie mwenyewe? Kwa nini mwathirika huyu asiye na hatia wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kudhoofika kwa njaa hakulindwa hadi akawa shabaha ya chakula cha tai?

Kwa upande mwingine, picha hiyo imechapishwa tena mara nyingi na imenakiliwa katika matangazo kwa mashirika kadhaa ya misaada yasiyo ya kiserikali (NGOs), ambayo yalichangisha fedha za kuwanunulia wakimbizi chakula.

Kwa maoni ya wengi, mwanadamu yeyote hangeweza kutazama picha hii bila kuuliza maswali. Kwa nini Carter hakumfukuza tai badala yake akasubiri pate picha? Vipi kama tai angeanza kumla yule mtoto, Carter angepiga picha wakati akiliwa? Kwa nini hakumfukuza yule tai?

Ni kwa jinsi gani Carter alimruhusu tai asogee karibu hivyo bila kufanya jambo lolote kumlinda mtoto? Alifanya nini baada ya kupiga picha hiyo? Kwa vile Carter aliamua kuchukua muda wa kutosha kupiga picha hiyo, dakika ambazo huenda zilikuwa muhimu wakati huu ambao mtoto alikuwa karibu na kifo, ilikuwa ni muhimu zaidi kupiga picha hiyo badala ya kumwokoa?

Baadhi ya marafiki zake na walimwengu wengine walimlaumu sana kutokana na picha hiyo. Wakosoaji wakawa wengi, wakisema mtoto yule aliyekuwa akielekea kwenye kituo cha msaada wa chakula, aliishiwa nguvu, akadondoka chini kupumzika, ndipo tai alipotua karibu yake huko macho ya tai huyo yakimwangalia mtoto huyo. Carter alichukua dakika 20 akisubiri kupiga picha, akitaka kupiga picha bora zaidi, kabla ya kumfukuza ndege huyo.

Hata hivyo, Gazeti la 'Times' lilitoa taarifa na kusema kuwa msichana huyo, baada ya kupumzika, aliweza kufika kwenye kituo cha chakula, lakini zaidi ya hapo hakuna anayejua kilichompata.

Kwa sababu ya hili, Carter alipigwa na maswali mengi juu ya kwa nini hakumsaidia mtoto huyo bali alimtumia tu kupata picha.

Gazeti la 'St. Petersburg Times' la Florida nchini Marekani liliandika hivi: "Mwanamume (Carter) anayerekebisha lensi yake ili kupata picha inayomfaa ya mateso yake (mtoto), anaweza pia kuwa tai mwingine kwenye eneo hilo."

Msanii wa filamu Dan Krauss wa Marekani alinukuliwa akisema: "Katika picha yake maarufu ya tai akimvizia mtoto wa Sudan, nilianza kuona mfano wa hali yake ya akili iliyojaa matatizo."

Shutuma na masuto dhidi mpigapicha yalikuwa mabaya kiasi kwamba hata familia yake ilianza kuhisi kuhuzunika kiasi kwamba binti wa Carter, Megan, alisema: "Namwona baba yangu kama mtoto anayeteseka. Na ulimwengu wote ni tai." Aliamini kuwa baba yake anaonewa kwa jambo jema alilofanya kuonyesha ulimwengu madhila ya njaa ya Sudan.

Jumatano ya Julai 27, 1994, ikiwa ni miezi minne baada ya kutunukiwa Tuzo ya Pulitzer, Carter alijiua kwa sumu ya kaboni monoksaidi akiwa na umri wa miaka 33.

Katika barua aliyoandika akiacha ujumbe wa kujiua kwake, Carter aliandika: Samahani sana. Maumivu ya maisha yanashinda furaha hadi furaha inatoweka ... huzuni ... bila simu ... pesa za kupangisha ... pesa za matunzo ya watoto ... pesa za madeni ... pesa! Nasumbuliwa na kumbukumbu mbaya za mauaji na maiti na hasira na maumivu ... maumivu ya watoto wenye njaa au waliojeruhiwa, wazimu wenye furaha, mara nyingi polisi wauaji ... nakwenda kuungana na Ken kama nina bahati hiyo..."

Katika barua hiyo Carter alimzungumzia Ken Oosterbroek aliyekuwa mpigapicha mwenzake wa gazeti la kila siku la 'The Star' la Johannesburg, Afrika Kusini.

Ken aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa na Carter mashariki mwa Johannesburg, Aprili 18, 1994, zikiwa ni siku tisa kabla ya uchaguzi mkuu wa kwanza nchini humo wa Aprili 27, 1994.

Polisi walisema mwili wa Carter na barua kadhaa alizowaandikia marafiki na familia zilikutwa kwenye gari lake lililokuwa limeegeshwa katika kitongoji cha Johannesburg. Walisema uchunguzi ulionyesha alikufa kwa sumu ya kaboni monoksaidi.

Desmond Tutu, aliyekuwa Askofu mkuu wa Anglikana Cape Town, Afrika Kusini, aliandika kuhusu Carter: “Na tunajua kidogo kuhusu gharama ya kuwa na kiwewe ambayo iliwafanya wengine kujiua, kwamba, ndiyo, watu hawa walikuwa wanadamu wakifanya kazi katika hali ngumu zaidi.”

Lakini nini hasa kilitokea. Kevin Carter ni nani hasa? Aliibukaje hadi kuwa mpigapicha maarufu duniani? Alitokaje Afrika Kusini hadi Sudan alikopiga mojawapo ya picha maarufu zaidi duniani kwa mwaka 1993 na 1994?

Alikutanaje na mtoto huyo? Nini kilimtokea huyo mtoto baada ya kupigwa picha na Carter? Aliondokaje Sudan kurudi Afrika Kusini? Kwanini alisutwa kwa kazi nzuri aliyofanya ya kuuhabarisha ulimwengu kuhusu njaa ya Sudan? Alifanya nini katika zile siku na dakika za mwisho za maisha yake? Kwa nini aliamua kujiua?

Maswali haya na mengine mengi yatajibiwa katika mfululizo wa simulizi hii inayoendelea kesho.