Plan international yatoa baiskeli 2,000 kaya maskini

Eva John mwanafunzi wa shule ya Sekondari Kisesa akikabidhiwa baiskeli na mkuu wa wilaya ya Geita, Wilson Shimo ili kumpunguzia adha yakutembea umbali wa zaidi ya km 10 kila siku kwenda shule. Baiskeli hizo zimetolewa na shirika la Plan international kwa msaada wa serikali ya watu wa Canada

Muktasari:

Ili kukabiliana na changamoto ya kutembea umbali mrefu na kusababisha baadhi ya wanafunzi wa kike kuacha masomo kwa kurubuniwa na wanaume, shirika lisilo la kiserikali la Plan international limetoa msaada wa baiskeli 2000 ili kuwawezesha mabinti kupata elimu.

Geita. Shirika lisilo la kiserikali la Plan International Tanzania limetoa msaada wa baiskeli 2,000 kwa wanafunzi wakike wanaotoka katika familia duni, ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule.

Akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli hizo leo Desemba 9, Mkurugenzi wa Miradi wa Plan International Tanzania, Peter Mwakabwale amesema baiskeli hizo ni moja ya utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wasichana wa rika balehe kuendelea na masomo (KAGIS) unaofadhiliwa na Serikali ya watu wa Canada katika mikoa ya Geita na Kigoma.

Amesema katika utekelezaji wa mradi wamebaini umbali mrefu ni moja ya changamoto zinazo kwamisha ndoto za wasichana kuendelea na masomo, hivyo wengi kujikuta wakiingia kwenye vishawishi na hatimaye kupoteza ndoto zao za elimu.

Baiskeli hizo zitatatolewa kwa awamu tofauti ambapo kwa kuanza wametoa 500 zitakazo gaiwa kwa mabinti wa wilaya tatu za mikoa ya Geita na Kigoma.

“Umbali mrefu wanaotembea kutoka nyumbani kwenda shule umewafanya wakate tamaa na wamekuwa na hofu ya kuadhibiwa wanapochelewa kufika shule.

“Hizi changamoto zimewafanya wengine kuacha shule, tumetoa baiskeli hizi ili tuwatengenezee mazingira rafiki, salama na wezeshi waweze kusoma na kutimiza ndoto zao,” amesema Mwakabwale.

Akishukuru kupata baiskeli, Eva John mwananfunzi wa shule ya Sekondari Kisesa iliyopo Wilayani Geita, amesema umbali mrefu wa zaidi ya kilometa tisa wanazotembea kila siku kwenda shule zimesababisha wanafunzi kurubuniwa kwa kupewa lifti kwa malipo ya kufanya mapenzi na dereva bodaboda.

Mbali na kurubuniwa wawapo njiani pia wanakumbana na hatari ya wanyama wakali kama fisi hivyo kulazimika kuchelewa kutoka nyumbani mapema na kukosa vipindi vya asubuhi shuleni.

Mmoja wa wazazi waliohudhuria ugawaji wa baiskeli, Jamila Seleman mkazi wa Igenge kata ya Ihanamilo, amesema kutokana na umbali mrefu wanafunzi walilazimika kuingia kwenye mahusiano na wanaume mtaani ili wapewe pesa za nauli na kujikuta wanapata ujauzito na kukatisha ndoto zao za kupata elimu.

Naye Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Ihanamilo, Salum Mkumala amesema baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo hulazimika kutembea zaidi ya kilomita 10 kila siku kwenda shule hivyo msaada wa baiskeli utawasaidia kufika shule mapema na pia wataweza kuhudhuria vipindi vya ziada jioni.

Akigawa baiskeli hizo Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo aliyemwakilisha mkuu wa mkoa huo Martine Shigela amesema zitasaidia wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kufika shule mapema na kutaka zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.


Aidha ameitaka jamii kuacha mtazamo hasi wa kuwa msichana hapaswi kwenda shule na badala yake waungane kuhakikisha watoto wa kike wanapata mazingira salama na wezeshi ya kujifunzia.