Polisi ajiua kwa risasi akiwa nyumbani kwa mpenzi wake
Muktasari:
Konstebo Samweli Kaziyote (24) wa Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Mbeya, alijiua kwa kujipiga risasi baada ya mzozo na mpenzi wake. Kamanda wa Polisi, Benjamin Kuzaga, alithibitisha tukio hilo na mwanamke anashikiliwa kwa mahojiano zaidi.
Mbeya. Askari polisi wa Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Mbeya, Konstebo Samweli Kaziyote (24), amefariki dunia baada ya kujipiga risasi kidevuni kwa kutumia bunduki aliyokuwa akitumia kwenye lindo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga ameieza Mwananchi Digital leo Jumatano Oktoba 4, 2023 kwamba polisi huyo mwenye namba J. 2596 alijiua saa 2:15 usiku wa kuamkia leo akiwa nyumbani kwa mpenzi wake baada ya kutokea mzozo kati yao.
“Marehemu akiwa kwenye eneo lake la lindo kulitokea mzozo kati yake na mpenzi wake jambo lililomfanya kuacha lindo na kuchukua silaha na kwenda kujiua ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi mwanamke huyo Mtaa wa Mzumbe, Forest ya zamani,” amesema.
“Kwa sasa bado tunaendelea na uchunguzi wa kina huku mwanamke (jina tunalihifadhi kwa ajili ya uchunguzi) anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi.”
Akizungumzia tukio hilo, mkazi wa Mtaa wa Forest,, Anjelina Peter amesema kuna haja kwa Jeshi la Polisi kuweka utaratibu wa kutoa elimu hususan kwa kuwatumia wanasaikolojia ili kuthibiti matukio ya watu kujiua.
“Hili ni kama tukio la pili nimesikia tangu nifike Mbeya, lipo la askari kujinyonga na hili na kujiua kwa kujipiga risasi kutokana na wivu wa mapenzi ”amesema.
Tukio hili linakuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kukaririwa akisema kwamba Serikali itaandaa utaratibu wa elimu ya afya ya akili na saikolojia ili kudhibiti matukio ya watu kujiua au kufanya mauaji.