Polisi Kiteto yanasa shehena ya dawa za kulevya

Jeshi la Polisi Kiteto lakamata shehena ya dawa za kulevya aina ya mirungi bunga 94 sawa na kilo 54.1. Picha na Mohamed Hamad Kiteto

Muktasari:

  • Imedaiwa kuwa watuhumiwa walikutwa na bunda 94, za mirungi sawa na kg 54.1 ambazo zilikuwa kwenye pikipiki isiyo na namba za usajili ikiwa na chasesi No MD2B1SBY64WJ87799 aina ya boxer ya rangi nyeusi.

Kiteto. Jeshi la Polisi wilayani Kiteto limekamata shehena ya dawa za kulevya aina ya mirungi bunda 94, ambazo ni sawa na kilo 54.1.

Dawa hizo zinadaiwa kupakiwa katika pikipiki aina ya boxer ya rangi nyeusi, isiyokuwa na namba za usajili.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne Novemba 14.2023 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, ACP George Katabazi ambapo pamoja na mambo mengine, amethibitisha dawa hizo kuwa aina ya mirungi.

"Tumekamata bunda 94 sawa na kilo 54.1 za mirungi zilizokuwa zinasafirishwa kwenye pikipiki na wahusika baada ya kuona wanafuatiliwa na Polisi walitelekeza pikipiki na dawa hizo, mpaka sasa tunaendelea kuwasaka," amesema SCP Katabazi.

Amesema watuhumiwa walionekana eneo la Mji Mdogo wa Matui Kiteto na kwamba pikipiki hiyo na mzigo huo wa dawa hizo, vinashikiliwa na jeshi hilo.

"Kiteto ni moja ya maeneo ambayo dawa za kulevya zinapitishwa kila mara...kuna maeneo mengine ambayo Polisi tumebaini kama vile Wilaya ya Babati, Minjingu, kuelekea Dodoma na Singida...kuna njia ya Simanjiro hadi Kiteto tunapowabana huku wanapitia njia za pembeni," amesema ACP Katabazi

Amesema watuhumiwa watasakwa na Jeshi la Polisi mpaka wapatikane kwani wanafahamika akisema ni bora wajisalimishe wenyewe kwenye kituo cha Polisi ili sheria ifuate mkondo wake mapema kuliko kujichelewesha wenyewe.

"Nitoe rai kwa wananchi wa Kiteto na Mkoa wa Manyara kwa ujumla kwamba Jeshi la Polisi tumejipanga vizuri njia zote tumeziba Babati Simanjiro hadi Kiteto tumeziba tutaendelea kuwakamata na kuwafikisha mahakamani," amesisitiza SCP Katabazi

Amesema watu wote wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya hatowaonea muhali... watakamatwa na sheria itafuata mkondo wake.

RPC huyo amewataka wananchi kujue madhara ya dawa za kulevya na kwamba Serikali imekataza matumizi yake, ikiwemo mirungi ambayo inaathari zaidi vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.