Polisi: Padri aliyekutwa kwenye tenki anaweza kuwa amejiua

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio la kifo cha Paroko wa Parokia ya Mbezi Mshikamano, Padri Francis Kangwa.


Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio la kifo cha Paroko wa Parokia ya Mbezi Mshikamano, Padri Francis Kangwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne Aprili 19, 2022 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro imeeleza kuwa uchunguzi wa awali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zimeonyesha dalili kuwa padre huyo ambaye ni raia wa Zambia anaweza kuwa amejiua.

Padri huyo alikutwa amefariki ndani ya tenki kubwa la maji lililopo nyuma ya nyumba ya makazi ya mapadri Mtaa wa Sokoine katika jengo la Ottoman jijini Dar es Salaam.

“Padri huyo alifika katika kanisa la St. Joseph lililopo mtaa wa Sokoine Aprili 12, 2022 kwa ajili ya ibada maalum, na mara baada ya ibada hiyo alielekea kwenye makazi ya Mapadri kujipumzisha lakini hakuonekana mpaka Aprili 15 alipokutwa amefariki eneo hilo.

“Uchunguzi wa awali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kiuchunguzi unaonesha dalili kwamba Padri huyo anaweza kuwa amejiua” imeeleza taarifa hiyo.

Taarofa hiyo imeeleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini sababu halisi iliyopelekea kifo cha Padri huyo.