Polisi wa Kenya auawa Tanzania

Picha ya Mtandao

Muktasari:

  • Habari kutoka wilayani Rombo zilizopatikana jana, zilieleza kuwa polisi huyo aliuawa katika eneo la Mbomai chini kwa kuchomwa kisu, kwa kile kinachoelezwa kuwa kiini chake ni wivu wa mapenzi.
  • Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agness Hokororo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo yaliyotokea Mei 13 mwaka huu.

Moshi. Askari wa Jeshi la Polisi nchini Kenya, John Munyoko (55), ameuawa kwa kuchomwa kisu na raia wa Tanzania, akiwa katika eneo la Tarakea wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Habari kutoka wilayani Rombo zilizopatikana jana, zilieleza kuwa polisi huyo aliuawa katika eneo la Mbomai chini kwa kuchomwa kisu, kwa kile kinachoelezwa kuwa kiini chake ni wivu wa mapenzi.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agness Hokororo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo yaliyotokea Mei 13 mwaka huu.

“Hiyo siku saa 4:00 usiku maeneo ya Mbomai chini kuna askari wa Jeshi la Polisi Kenya, anafanyia kazi kituo cha Elasit Kenya alikuja Tanzania akawa anakunywa pombe kwenye grosari moja,”amesema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, polisi huyo alikuwa akinywa pombe na mwanamke mmoja Mtanzania, wakati wakiendelea kunywa, alitokea mwanamme mmoja ambaye alimchoma kisu mwanamke huyo.

“Alimchoma kisu mwanamke ambaye alikuwa akinywa pombe na huyo mkenya yeye hakufariki. Alimchoma mbavuni na ziwa la kushoto na yuko Huruma Hospitali,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Hokororo amesema baadaye mwanaume huyo alimshambulia kwa kisu polisi huyo na kumsababishia majeraha mabaya, ambapo raia wema walijitokeza kutoa msaada lakini mtuhumiwa alitokomea kusikojulikana.

“Raia wema walijitahidi kuwasaidia na pia askari wa Kenya walikuja na kumchukua lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia akipelekwa hospitali,” amesema mkuu huyo wa wilaya na kuongeza;-

“Kinachoendelea ni pande zote mbili kwa sababu haya ni mauaji kwa hiyo sisi huku Tanzania vyombo vya ulinzi usalama vinaendelea kumtafuta na Kenya wanaendelea kumtafuta.”

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi wenye taarifa sahihi za mahali alipo mtuhumiwa huyo, wavisaidie vyombo vya dola kwa kutoa taarifa ili mtuhumiwa huyo aweze kukamatwa na kushitakiwa.