Polisi wakamata bodaboda 118 ndani ya siku mbili

Wednesday August 04 2021
bodabodapic
By Tatu Mohamed

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limefanikiwa kukamata bodaboda 118 katika siku mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Agosti 4, 2021 Kamanda wa polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Jeshi hilo linaendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kuzuia makosa ya kijinai na kuwakamata wanaovunja sheria za ikiwa ni pamoja na kukamata waendesha bodaboda wanaokiuka sheria za usalama barabarani.

Amesema operasheni ya kukamata bodaboda ilianza Agosti 2 na imefanikiwa kukamata pikipiki (Bodaboda) 118 zilizofanya makosa mbalimbali ya usalama barabarani.

Ameyataja makosa hayo kuwa ni kutovaa kofia ngumu(Helment) pikipiki 43, kupakia abiria zaidi ya mmoja (mshikaki) pikipiki 17, kutokuwa na leseni ya udereva pikipiki 20, kupita taa nyekundu Pikipiki 24, Pikipiki mbovu nane na pikipiki sita zilikamatwa kwa kosa la kupita barabara ya mwendokasi DART.

"Ukamataji huu ni endelevu na hizi pikipiki sita zilizopita barabara ya mwendokasi, madereva wake watafikishwa mahakamani na pikipiki zilizokamatwa kwa makosa mengine ya usalama barabarani zitakaguliwa na kulipa faini," amesema.

Advertisement