Polisi wanasa mabasi ya shule yaliyokwepa ukaguzi Morogoro
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Morogoro, Gabriel Chiguma akizungumza jambo na waandishi wa habari wakati wa zoezi la ukaguzi wa magari ya kubeba wanafunzi Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeanza operesheni ya kuyakamata mabasi ya shule yaliyoshindwa kujitokeza kwenye ukaguzi wa hiari wakati wa likizo.
Morogoro. Baada ya baadhi ya wamiliki wa mabasi ya shule kupuuza wito wa kuyapeleka kwenye ukaguzi wa hiari wakati wa likizo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeanza operesheni ya kuyakamata magari hayo, huku mabasi 15 kati ya 25 yaliyokaguliwa yakibainika kuwa na kasoro zinazohatarisha usalama wa wanafunzi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 9, 2026 mkoani hapa, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro, Gabriel Chiguma amesema ukaguzi wa hiari ulitangazwa katika kipindi chote cha likizo ili kutoa nafasi kwa shule kukagua mabasi yao bila kuathiri ratiba za masomo.
Chiguma amesema taarifa za ukaguzi zilifikishwa kwa shule kupitia barua rasmi na ujumbe wa WhatsApp, zikiwaalika kupeleka mabasi yao kwa ukaguzi.
Hata hivyo, amesema shule chache ndizo zilizoitikia wito huo, hali iliyolazimu Jeshi la Polisi kuanza operesheni maalumu ya kuyakamata mabasi ambayo hayakufikishwa kwa ukaguzi wa hiari ili yakaguliwe kwa lazima na hatua stahiki zichukuliwe pale yatakapobainika kukiuka sheria au kutokidhi viwango vya usalama.
Amesema kati ya mabasi 25 yaliyokaguliwa katika operesheni hiyo, 15 yamezuiwa kuendelea kutoa huduma baada ya kubainika kuwa na hitilafu mbalimbali, ikiwemo ubovu wa mifumo ya breki, injini, uchakavu wa miili ya magari pamoja na kutokidhi matakwa ya kisheria kuhusu upakaji wa rangi.
"Mabasi hayo yatalazimika kufanyiwa matengenezo na kurejeshwa kwa ukaguzi mwingine. Yataruhusiwa kuendelea na huduma baada ya kuthibitishwa kuwa yanakidhi viwango vya usalama vinavyotakiwa," amesema Chiguma.
Aidha, amepiga marufuku matumizi ya magari binafsi ya kukodi kusafirisha wanafunzi, akisema hayana sifa za kisheria kufanya kazi hiyo na yanaweza kuhatarisha usalama wa watoto.
Amewataka wazazi kuacha kuchangia matumizi ya magari yasiyoidhinishwa na badala yake kuhakikisha watoto wao wanatumia usafiri unaokidhi matakwa ya sheria na viwango vya usalama.
Mmoja wa madereva waliokaguliwa, Thompson Patrick, amesema ukaguzi huo una manufaa makubwa kwa madereva na wamiliki wa mabasi kwa kuwa unawasaidia kubaini mapema kasoro zinazoweza kusababisha ajali.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, mabasi 10 kati ya 25 yaliyokaguliwa yamekidhi viwango vya usalama na kuruhusiwa kuendelea na huduma, huku operesheni hiyo ikiendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro ili kuhakikisha mabasi yote ya shule yanayosafirisha wanafunzi yanakaguliwa na kuzingatia sheria za usalama barabarani kabla ya muhula mpya wa masomo kuanza.