Polisi waonya watakaojihusisha na ukeketaji Mara
Muktasari:
Jeshi la Polisi mkoani Mara limesema halitasita kuwachukulia hatua kali wote watakaojihusisha na vitendo vya ukeketaji katika mkoa huo wakati wa likizo ya mwisho wa mwaka.
Musoma. Jeshi la Polisi mkoani Mara limetoa onyo kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya ukeketaji wakati wa likizo ya mwisho wa mwaka likidai atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Onyo hilo limetolewa leo Alhamisi Novemba 30, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase wakati alipokuwa akiongea na Mwananchi Digital juu ya madai ya kuwepo kwa maandalizi ya ukeketaji kwa baadhi ya koo mkoani humo.
“Ukeketaji ni kosa kisheria, mbali na kuwa ni ukatili na unyayasaji wa kijinsia hivyo sisi kama wasimamizi wa sheria na haki za binadmau hatutakuwa tayari kuona mtoto wa kike akifanyiwa ukatili na kuvunjiwa haki zake kwa kisingizio cha mila na desturi,"amesema
Amesema ili kuwa na matokeo chanya katika mapambano dhidi ya ukeketaji jeshi hilo kupitia madawati yake ya jinsia limekuwa likitoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukeketaji na kwamba wanaamini elimu imefika kwa jamii nzima hivyo atakayeamua kuendeleza vitendo hivyo atakuwa anafanya kwa maamesema
“Hakuna asiyejua kuwa ukeketaji ni kosa kisheria na pia ni ukatili kwa mtoto kwasabau dawati letu limekuwa mstari wa mbele kutoa elimu katika jamii kwa kushirikiana na wadau wengine wa haki za binadamu hivyo naamini tukichukua hatua hatutakuwa tunamuonea mtu yeyote niommbe tu ushirikiano kwa wananchi wote,”amesema Kamanda Morcase
Inaadaiwa maandalizi ya ukeketaji tayari yameanza huku, walengwa wakuu wakiwa ni wanafunzi wa kike hasa wa shule za msingi.
“Yapo mambo mengi yanayofanyika ili kuruhusu tohara kwa ujumla ifanyike na panapokuwa na tohara humo humo na ukeketaji huwa unafanyika,”amesema Mwita Nchagwa mkazi wa Nyabange Wilaya ya Butiama
“Kuna namna ya kuangalia kama mwaka huu tufanye au tuache na hii inafanyika kimila zaidi lengo ni kutaka kujua kama mwaka hauna mikosi maana mkilazimisha wanaokwenda jando watakufa,”amesema Juma Werungu
Meneja Miradi wa kituo cha kupinga ukeketaji cha Masanga kilichopo wilayani Tarime,Valerian Mgani amesema hadi sasa bado hawajabaini uwepo wa maandalizi ya ukeketaji kwa mwaka huu kwa upande wa Tanzania ingawa upo uwezekano wa maandalizi hayo kuanza kwani hufanyika kwa usiri mkubwa.
“Haya mapambano huwa tunayafanya kwa ushirikiano na tayari tumebaini wenzetu wa nchi jirani hasa maeneo yanayopakana na wilaya ya Tarime kwa kata za Susuni na Mwema maandalizi yanaendelea sasa kwetu sisi hii ni 'alarm' tunafanya ufuatiliaji wa karibu ili kuwanusuru watoto wa kike,”amesema Mgani
Amesema upo uwezekano wa watoto kutoka Tanzania kuvuka mpaka na kwenda kufanyiwa ukeketaji nchi jirani kutokana na muingiliano wa tamaduni na mila hivyo maandalizi ya ukeketaji kwa nchi jirani yana madhara ya moja kwa moja kwa upande wa Tanzania pia.