Tanzania yaita nguvu ya wadau kutokomeza ukeketaji
Dar es Salaam. Tanzania imewaita wadau ndani na nje ya nchi kuweka nguvu ya pamoja, kuharakisha mabadiliko yanayohitajika kutokomeza matukio ya ukeketaji kwa wanawake na wasichana.
Jambo la kusikitisha, licha ya wataalamu wa afya kufahamu athari za ukeketaji, kati ya wanawake na wasichana milioni 200 waliokeketwa duniani milioni 20 walifanyiwa dhuluma hiyo na wataalamu wa afya.
Ugumu wa taifa moja moja kusimama kutokomeza vitendo vya ukeketaji kutofanikiwa kwani changamoto kubwa kwa sasa ni wanawake na wasichana kuvushwa kwenda nchi za jirani kukeketwa.
Leo Oktoba 9, 2023 kwenye mkutano wa kimataifa wa kutokomeza ukeketaji ukiwa na kaulimbiu 'Mabadiliko katika kizazi' Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima amesema matukio ya ukeketaji yanahitaji kukabiliwa kwa uzito mkubwa.
"Tanzania inatoa wito kwa jamii zote wadau wetu wa ndani na nje ya nchi pamoja na nchi zingine kuungana nasi katika kuharakisha mabadiliko yanayohitajika ili kubadilisha maisha ya wanawake na wasichana," amesema.
Dk Gwajima amesema jambo linalosababisha wanawake na wasichana kuendelea kupitia mathila ya ukeketaji, ni mila zenye madhara hivyo nguvu ya kutokomeza isipowekwa kuna hatari ya kutowapata wanawake na wasichana wenye elimu.
Wasiwasi wa Dk Gwajima unajikita pia katika upatikanaji wa rasilimali fedha kuendesha miradi ya kutoa elimu ya kutokomeza ukatili huo pamoja na wanaume kutoweka nguvu kupambana na ukeketaji badala yake kuwaachia wanawake pekee.
Amesema mataifa yote duniani yanahitaji kuwa na nguvu ya pamoja kulinda wanawake milioni 68 duniani walio kwenye hatari ya kukeketwa, milioni 50 wakitokea nchi za Afrika.
Kuendelea kwa matukio ya ukeketaji nchini, Dk Gwajima amesema kutachochea Tanzania kutofikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs 2030 ya kutokomeza ukeketaji.
Akizungumzia suala la ukeketaji kwa mtindo wa kuvusha watoto na wanawake mipakani na kwenda kuwakeketa, Dk Gwajima amesema tatizo hilo lipo Tanzania kwa kiwango kikubwa.
"Tatizo lipo kubwa na limefanyiwa kazi tuna wataalamu wetu mipakani na kwenye jamii hakuna mtoto anayeweza kuvushwa kuingizwa nchi nyingine lazima mama au mtu mwenye mtoto aeleze anakwenda wapi na mtoto,"amesema.
Shirika la Men End FGM la nchini Kenya mwaka jana lilionyesha kuwa ukeketaji nchini Kenya hufanyika kwa asilimia 21 nchini Tanzania na asilimia 10 ya matukio ya Tanzania yakifanywa nchini Kenya.
Zeituna Abdullahi wa Shirika la Merti Intergraed ya nchini Kenya, amesema matukio ya ukeketaji yanaendelea kutokana na matukio hayo kufanywa kuwa ya kidini.
Balozi wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Janet Sallah Njie, amesema ili kutokomeza matukio ya ukeketaji kwa watoto wa kike, lazima kuwe na mkakati wa kidunia wa kuzuia watoa huduma za afya kufanya ukeketaji.
Pia amesema upatikanaji mgumu wa takwimu za matukio ya ukeketaji nayo ni changamoto ya kutokafikiwa malengo ya kutokomeza ukeketaji.
Mkakati uliopo Tanzania
Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji 2020/2021-2024/2025, unaonyesha Tanzania imejiwekea lengo la kupunguza kiwango cha ukeketaji kutoka asilimia 10 ya mwaka 2015/2016 hadi kufika asilimia 5 mwaka 2024/2025.
Mkakati huo utafanikiwa endapo wasichana na wanawake watakataa kukeketwa, familia kukataa matukio hayo, msaada wa huduma za wahanga wa ukeketaji zitapatikana kwa wakati na utaratibu wa wadau kushugulikia masuala ya ukeketaji yataimarishwa
Kwa takwimu za Kituo cha Sheria na haki za binadamu Tanzania mwaka 2020 zaidi ya watoto 700 waliokolewa dhidi ya ukeketaji.
Takwimu na athari za ukeketaji
Baadhi ya athari za ukeketaji ni maumivu makali, kutokwa na damu nyingi, uvimbe wa tishu na viungo vya uzazi, matatizo ya mkojo, vifo, maambukizi ya magonjwa na homa kali.
Kwa upande wa takwimu, Taarifa ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania 2015/2016 matukio hayo yameenea katika mikoa ya Manyara asilimia 58, Dodoma asilimia 47, Arusha asilimia 41, Mara asilimia 32, Singida asilimia 31, Tanga asilimia 14.