Watoto 16 Tanzania kushiriki mkutano Switzerland
Muktasari:
- Wanafunzi 16 wamekabidhiwa bendera ya Tanzania leo kwa ajili ya kushiriki mkutano wa watoto nchini Switzerland utakaojadili masuala ya mazingira na haki za watoto.
Morogoro. Wanafunzi 16 kutoka shule ya Msingi na Sekondari ya Elu mkoani Morogoro wanatarajiwa kwenda Davos nchini Switzerland kushiriki katika mkutano wa Jukwaa la Watoto linalolenga kujadili masuala ya mazingira na haki za watoto.
Akizungumza leo Jumatatu Julai 17,2023 kwa niaba ya wenzake mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa, walipofika ofisini kwake kuaga kwa ajili ya safari hiyo na namna watakavyowakilisha Tanzania, mmoja wa wanafunzi hao, David Ishumi amesema wataenda kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa Kiafrika.
Ishumi amesema changamoto hizo ni pamoja na masuala ya ukatili, unyanyasaji wa kijinsia, ubaguzi wa rangi, kunyimwa haki ya kupata elimu, haki ya malezi bora na ukosefu wa amani kwa baadhi ya mataifa barani Afrika yanayowakabiliwa na masuala ya kivita.
Amesema majadiliano katika jukwaa hilo yatawawezesha kutengeneza kesho iliyo njema kwa watoto walio wengi barani Afrika, ambapo watahakikisha wanashiriki kikamilifu katika majadiliano ili kutambua namna mataifa mengine yanavyosimamia haki zao.
“Tunaenda kwenye mkutano wa watoto duniani, tunaenda kuwasilisha na kujadili hoja zetu kama watoto, shida tunazopitia na mahitaji tunayoyataka, tutawasilisha changamoto wanazopitia, tumeona baadhi ya nchi za Afrika zinakabiliwa na vita, watoto wanakufa kwa kukosa afya na chakula bora,”amesema.
Naye mwanafunzi Jackline Kisantos amesema, jukwaa hilo watajadili namna baadhi ya jamii zinazoendelea na ukeketaji kwa watoto wa kike na kuwanyima haki ya kupata elimu kwa kuwaozesha katika umri mdogo.
Mkurugenzi Shule ya Elu, Erasto Luanda amesema mkutano huo utafanyika kwa siku tisa, ukihusisha watoto 200 kutoka mataifa mbalimbali duniani, ambapo ushiriki wao umechagizwa na mashirikiano mzuri baina ya shule hiyo na baadhi ya mataifa mengine.
Amesema mkutano huo wa majadiliano ya masuala ya mazingira na haki za watoto wanashiriki kwa mara ya kwanza, na kwamba watapata fursa ya kujadili mambo kadhaa kuhusiana na uimara wa mahusiano baina ya mataifa ili kurejesha amani duniani, kujadili uchafuzi wa mazingira ili kuwanusuru kizazi kijacho na kasi ya ongezeko la joto duniani.
“Tunashiriki kwa mara ya kwanza katika jukwaa hili, nafasi hii tumeipata baada ya mahusiano mazuri tuliyonayo na mataifa mengine, mwaka 2015 tulishiriki jukwaa la maonyesho ya nyimbo za utamaduni nchini Ujerumani, awamu hii wametukumbuka pia, kwa Tanzania na Afrika sisi ndio wawakilishi pekee katika jukwaa,”amesema Luanda.
Akiwakabidhi bendera ya Taifa watoto hao, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa amewataka watoto hao wakawe mabalozi wazuri na kuitangaza Tanzania katika masuala ya Utalii na Utamaduni kwa kuhakikisha wanakuwa taswira ya watoto Watanzania kwa kushiriki kikamlifu katika majadiliano hayo.
Amewasisitiza kutumia jukwaa hilo kuwajenga kifikra na kutoa mchango wao kwenye malengo ya kidunia ya miaka thelathini ijayo yayolenga kulinda haki za watoto, uslama wa mazingira na masuala ya amani duniani.
“Natamani mwende mkaonyeshe jinsi tulivyo sisi Watanzania kwa mataifa mengine, sisi Watanzania ni watu wenye upendo na mashirikiano mazuri kama mnavyofundishwa kwenye historia, nendeni mkashiriki kikamilifu, muwe mabalozi wazuri wa taswira ya Tanzania na Afrika,”amesema.