Polisi watoa kauli gari lililotumbukia baharini, dereva asalimika

Muktasari:

  • Gari aina ya Toyota Landcruiser Prado limetumbukia katika Bahari ya Hindi eneo la  ufukwe wa Coco huku polisi wakieleza kusubiri afya ya dereva wa gari hilo kuimarika ili waanze uchunguzi.


  

Dar es Salaam. Gari aina ya Toyota Land Cruiser Prado limetumbukia katika Bahari ya Hindi eneo la  ufukwe wa Coco huku polisi wakieleza kusubiri afya ya dereva wa gari hilo kuimarika ili waanze uchunguzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni, Ramadhani Kingai ameieleza Mwananchi Digital leo Jumanne Oktoba 5,2021 kuwa  hakuna madhara yoyote yaliyotokana na ajali hiyo baada ya mtu huyo  kuokolewa.

Amesema wanasubiri afya yake iimarike ili wafanye uchunguzi wa tukio hilo kwa kuwa dalili zinaonyesha alikuwa ni mtu mwenye mawazo au tatizo la akili.

Polisi watoa kauli gari lililotumbukia baharini, dereva asalimika

"Kule alipokuwa anakwenda kulikuwa hakuna barabara, kama mtu ni mzima huwezi kuona gari linakwenda baharini na wewe ukazidi kukanyaga mafuta," amesema Kingai.


Wakizungumzia tukio hilo mashuhuda wanadai tukio hilo lilitokea jana saa saba mchana baada ya kuliona gari kwenye maji na alikuwepo dereva pekee ambaye walifanikiwa kumuokoa na kumkimbiza hospitali baada kunywa maji mengi katika jitihada za kujiokoa.

“Nilipigiwa simu nikaambiwa kuna gari aina ya Landcruiser  limeingia baharini nilichukua pikipiki na nikafika katika eneo hili niliwakuta kikosi kazi tayari wameshamtoa yule bwana na tayari wamemkimbiza hospitali," amesema mwenyekiti wa uokoaji na utunzaji mazingira Coco Beach, Ahmed Abdallah.

Vijana waliokuwa karibu na eneo hilo walitumia takribani saa mbili kulitoa  gari kwenye maji japo haikuwa kazi rahisi kutokana na eneo lilipotumbukia.

“Ilichukua muda kulitoa gari, tulitumia zaidi ya saa mbili na ilitokana na  hali ya upepo na maji yanakwenda kasi lakini kwa sababu vijana wanaielewa vizuri bahari wakaona na kusoma jiografia ya bahari na wakaona eneo muafaka pakutolea gari," amesema.