Polisi wavunja mkutano wa Chadema, 30 wakamatwa

Polisi wavunja mkutano wa Chadema, 30 wakamatwa

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limevunja mkutano wa kujadili Katiba Mpya ulioandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) pamoja na kuwakamata makada 30 kwa madai ya kufanya mkutano wa hadhara bila kibali.

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limevunja mkutano wa kujadili Katiba Mpya ulioandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) pamoja na kuwakamata makada 30 kwa madai ya kufanya mkutano wa hadhara bila kibali.

Hata hivyo, Chadema wamepinga madai hayo ya kufanya mkutano wa hadhara, wakisema ulikuwa in mkutano wa ndani ambao kwa utaratibu hauhitaji kibali cha Polisi.

Akizungumza kwa simu leo Jumamosi Julai 17,2021, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi alisema wamevunja mkutano huo kwa kuwa haukuwa na kibali.

"Ni kweli tumezuia mkutano ulioandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema kwa ajili ya kudai Katiba mpya kwa kuwa hawakutoa taarifa Polisi na sisi kuwaruhusu kufanya mkutano huo," alisema Kamanda Ng'anzi.

Amesema Julai 16,2021 waliwaandikia Chadema barua ya kuzuia mkutano huo, lakini wengine hawakutii.

"Wale ambao hawakutii tumewakamata na mpaka sasa tunawashikilia watu 30 kwa ajili ya mahojiano. Wakithibitika kuna uwezekano tukawapeleka mahakamani," amesema.

Alipoulizwa sababu ya kuwakamata wakati walipanga kufanya mkutano wa ndani na sio wa hadhara, Kamanda Ng'anzi amesema matangazo ya mkutano huo yaliashiria mkutano wa hadhara.

"Haukuwa mkutano wa ndani, jana kulikuwa na gari la matangazo lililokuwa likihamasisha kila mwananchi kuhudhuria. Ilikuwa ni lugha ya kupaka sukari tu kwamba ni mkutano wa ndani, lakini ulikuwa wa hadhara.

"Ni mkutano wa ndani, lakini uliruhusu watu wote kuingia kwa mwanachama na asiye mwanachama," amesema.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi kwa simu, Msemaji wa Bavicha, Apolnary Margwe amesema hawakuwa na haja ya kuomba kibali kwa kwa kuwa ulikuwa ni mkutano wa ndani.

Amesema awali Polisi walifika katika baa ya Boma iliyopo Nyakato Sokoni na kukamata viongozi watatu waliokuwa wakifanya maandalizi kwa ajili ya mkutano huo.

Amewataja viongozi waliokamatwa kuwa ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Bavicha, Richard Kaunya, Mwenyekiti wa Bavicha mkoa wa Mwanza, Boniface Nkobe na mhamasishaji wao, Kamanda Paulina.

"Viongozi wetu wamekamatwa wakiwa wanafanya maandalizi ya mkutano ukumbini," amesema Margwe.

Awali, barua ya Polisi iliyopatikana mitandaoni na iliyosainiwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Ilemela, Shamila Mkomwa ya Julai 16, 2021 akionya Bavicha kutofanya mkutano huo kwa kuwa haukuwa na kibali.

"Kwa kuwa ofisi yangu haijapokea barua kutoka kwenu mkitoa taaarifa ya kufanyika mkutano huo na endapo mkutano huo utafanyika bila idhini yangu, tambua kabisa mkutano huo utakuwa batili," imesema sehemu ya barua hiyo.