Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi yanasa watuhumiwa 239 matukio ya uhalifu, mauaji, ubakaji

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Ijumaa Julai 3, kuhusu masuala mbalimbali ya usalama na matukio yaliyotokea mkoani humo.

Muktasari:

  • Watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni maalumu zilizofanyika kuanzia Juni mosi hadi Juni 30, 2026

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa 239 wanaotuhumiwa kuhusika na makosa mbalimbali yakiwamo ya mauaji, kujeruhi, ubakaji, kukutwa na silaha bila kibali pamoja na dawa za kulevya.

Watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni maalumu zilizofanyika kuanzia Juni mosi hadi Juni 30, 2026, zikiwa na lengo la kuimarisha ulinzi na usalama na kudhibiti vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, Julai 3, 2026 ofisini kwake jijini Mbeya, Kamanda wa Polisi mkoa huo, Benjamin Kuzaga amesema operesheni hizo zimezaa matokeo makubwa katika mapambano dhidi ya uhalifu.

"Katika kuimarisha ulinzi na usalama, Jeshi la Polisi lilifanya operesheni na misako mbalimbali katika kipindi cha Juni na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa makosa ya mauaji, ubakaji, kujeruhi, kukutwa na silaha bila kibali pamoja na dawa za kulevya," amesema.

Amesema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.

Katika hatua nyingine, Kamanda Kuzaga amesema watu watatu wanashikiliwa kwa tuhuma za kumuua bibi yao, Mary Mwasile (70), mkazi wa Kijiji cha Isongole, Kata ya Santilya, Wilaya ya Ileje kwa kumchoma kitu chenye ncha kali shingoni.

Kwa mujibu wa polisi, tukio hilo lilitokea Juni 28, 2026, saa 4:30 asubuhi, wakati marehemu alipokuwa ndani ya nyumba yake.

Watuhumiwa hao ni Yelle Mboya (27), mkazi wa Tunduma mkoani Songwe, Furaha Mboya (25) na Elisa Mboma (43), wote wakazi wa Isongole.

Kuzaga amesema kikosi maalumu cha kupambana na matukio ya mauaji kilianza uchunguzi baada ya tukio na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Amesema uchunguzi wa awali unaonesha mauaji hayo yanahusishwa na imani za kishirikina, huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Katika tukio tofauti, Jeshi la Polisi linawashikilia Shughuli Halezy (50), Shaban Matulu (36) na Baraka Mwaluswaswa (26), wote wakazi wa Lualaje, Wilaya ya Chunya, kwa tuhuma za kukutwa na silaha aina ya gobole bila kibali.

Watuhumiwa hao walikamatwa katika Kijiji cha Bintimanyanga, Kata ya Mafyeko, Tarafa ya Kipembawe, wakiwa na silaha hiyo, magobori 13 yaliyokuwa yakitumika kama risasi pamoja na fataki 15.

Kamanda Kuzaga amesema jeshi hilo linaendelea na operesheni katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo,  kwa lengo la kuzuia uhalifu na kuwafikisha wahusika mbele ya vyombo vya sheria.

Wakati huohuo, mkazi wa Kata ya Mabatini jijini Mbeya, Solomon Eliud ameliomba Jeshi la Polisi kurejesha utaratibu wa ulinzi wa jadi (sungusungu) ili kusaidia kudhibiti matukio ya uhalifu katika jamii.

Amesema pia kuna haja ya kuwepo kwa utaratibu wa lazima kwa wamiliki wa nyumba kutoa taarifa za wapangaji na wageni kwa viongozi wa Serikali za mitaa ili kudhibiti upangishaji holela unaoweza kuwapa nafasi wahalifu kujificha.

"Ni muhimu wamiliki wa nyumba wakatoa taarifa za wageni na wapangaji kwa viongozi wa maeneo yao badala ya kutanguliza masilahi ya fedha pekee. Hii itasaidia kuimarisha usalama," amesema.