Polisi yaongoza taasisi zinazolalamikiwa na wananchi

Muktasari:

  •  Ikiwa imetimia miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imelitaja Jeshi la polisi kama Taasisi kinara inayolalamikiwa zaidi na wananchi.



Dodoma. Ikiwa imetimia miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imelitaja Jeshi la polisi kama Taasisi kinara inayolalamikiwa zaidi na wananchi.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Septemba 9, 2022 na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya miaka 20 ya THBUB jijini Dodoma.

Mwaimu amesema kuwa malalamiko mengi kwa Jeshi hilo ni ya matukio ya watuhumiwa kudaiwa kufa au kuteswa wakiwa chini ya mikono ya polisi.

“Kwa sehemu kubwa ni malalamiko kwa Jeshi la polisi kwa sababu wao ndio mamlaka ya kukamata, kufanya upelelezi na kupeleka upelelezi huo kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na kufuatia hilo ndipo mwezi uliopita tulitoa tamko letu Dar es salaam na kutoa mapendekezo.

Malalamiko mengi yanakuwa sehemu ya ukamataji, ubambikizaji wa kesi na rushwa,” amesema Mwaimu.

Mwaimu amesema Taasisi nyingine zinazolalamikiwa ni pamoja mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuchelewa kutoa stahiki za wastaafu kwa wakati.

Pia, amesema malalamiko kama hayo huelekezwa kwa Mahakama, sehemu za kutolea huduma za afya na migogoro ya ardhi.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo, Mwaimu amesema shughuli mbalimbali zinatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 10 hadi 15, mwaka huu.

Amesema Septemba 10, wadau, wananchi na viongozi wa Tume watapanda miti ya vivuli na matunda katika eneo la Nkuhungu ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Mwenyekiti huyo amesema katika wiki hiyo yatafanyika maonesho ya mabanda ya Taasisi za umma na binafsi ambayo yataenda sambamba na kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kupokea malalamiko kuhusu wajibu na haki za binadamu na utawala bora.

Pia, amesema watumishi hao watatembelea maeneo walipozuiliwa watoto walio katika mkinzano na sheria mkoani Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Lindi ili kujionea uzingatiwaji wa haki za mtoto katika vituo husika.