Polisi yapiga maarufu watoto kupanda bodaboda

Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Iringa, Mossi Ndozero akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Wambi na Nyamalala kuhusu masuala ya usalama barabarani leo Alhamisi Aprili 6, 2023 wilayani Mufindi. Picha na Mary Sanyiwa.

Iringa. Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa na Mrakibu wa Polisi, Mossi Ndozero amepiga marufuku watoto wadogo chini ya miaka tisa kupanda pikipiki wakiwa pekee yao kwani inahatarisha usalama wao pindi wanapokuwa kwenye pikipiki hizo.

Akizungumza na wazazi katika Shule ya Msingi Wambi iliyopo katika Halmashauri ya Mji Mafinga, Ndozero amesema watoto chini ya miaka tisa hawapaswi kupanda kwenye pikipiki wakiwa peke yao bila kuwa na mtu mzima kwa ajili ya usalama wao.

Aidha amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto zetu za usafiri, pia Sheria ya Usalama Barabarani hairuhusu mtoto chini ya miaka hiyo kupanda pikipiki hizo kwani inahatarisha usalama wao kutokana na watoto hao kukosa uangalizi.

"Niwaombe wazazi kuacha tabia ya kuwapakia watoto kwenye pikipiki kwa sababu sheria ya usalama barabarani hairuhusu mtoto chini ya miaka tisa kupanda pikipiki na kama unampandisha basi lazima awe na mtu mzima wa kumuangalia," amesema Ndozero.

“Unampakia mtoto kwenye pikipiki halafu upepo unampuliza kisha anapata usingizi, anaweza kuondoka na kupoteza maisha. Hapo inakuwa hasara ni vizuri kumwangalia kwa umakini mkubwa watoto wetu ili wasipate madhara," amesema mkuu hiyo wa Polisi.

Katika hatua nyingine, Ndozero amewataka wazazi hao kuhakikisha wanawalinda watoto wao dhidi ya masuala ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji na ulawiti na kupata muda wa kukaa na watoto wao sanjari na kuwauliza changamoto ambazo wanazokutana nazo.

Kwa upande wa mmoja wa wazazi Richard Mgaya amesema kuwa wamepokea maelekezo ya mkuu huyo wa usalama barabarani watafanyia kazi kwa ajili ya kuwalinda watoto wao.

"Tumepokea Elimu kuhusu watoto chini ya miaka tisa kupanda pikipiki kwa sababu awali tulikuwa hatuyafahamu kwamba sheria ya usalama barabarani hairuhusu mtoto chini ya umri huo kupanda usafiri huo," amesema Mgaya.