Polisi yatangazia vita ‘panyarodi’

  • Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, wakati akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dodoma kuhusu hali ya usalama nchini. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Siku moja baada ya Bunge kutoa maelekezo kwa Serikali juu ya kuvikabili vikundi vya kihalifu vilivyoibuka baadhi maeneo ikiwemo jiji la Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni amesema hakuna atakayejihusisha na uhalifu atabaki salama.

Dar/Dodoma. Siku moja baada ya Bunge kutoa maelekezo kwa Serikali juu ya kuvikabili vikundi vya kihalifu vilivyoibuka baadhi maeneo ikiwemo jiji la Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni amesema hakuna atakayejihusisha na uhalifu atabaki salama.

Juzi wabunge waliomba kuahirishwa kwa shughuli za Bunge kwa muda ili kujadili, kadhia ya vikundi vya uhalifu vinavyoundwa na vijana maarufu ‘panya road’ wanaovamia, kujeruhi na kupora mali mbalimbali.

Miongoni mwa matukio ni lililotokea hivi karibuni mtaa wa Dovya Chamanzi, Wilaya ya Temeke ambapo vijana wakiwa na mapanga, nondo na marungu walivamia, kujeruhi na kuiba vitu mbalimbali vikiwemo simu, runinga na fedha.

Siku hiyo hiyo vijana hao walivamia maeneo ya Kawe Mzimuni, Dar es Salaam na kujeruhi, kupora mali na kusababisha kifo cha Maria Basso (24) mwanafunzi wan waka wa pili wa Shule ya Uandishi wa Habari Dar es Salaam (SJMC).

Akizungumza na wanahabari juzi jijini Dodoma Waziri Masauni alisema, wote waliojihusisha na vikundi ikiwemo Dar es Salaam mtandao wao unashughulikiwa.

“Sielezi mambo gani yamefanyika na jitihada zipi hata Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura hawezi kusema hapa, lakini juhudi zinafanyika,” alisema.

“Tumebaini wanaoongoza uhalifu ni wengi waliomaliza vifungo vyao, tunafanya maboresho katika mfumo wa magereza nchini. Mkakati wa Polisi unaweza kuchukua muda mfupi kukabiliana na haya ikiwa wananchi watatoa ushirikiano,”alisema Masauni.

Waziri Masauni alitoa pole kwa waliopatwa na majanga, na kuwataka kutambua kuwa vyombo vya dola viko imara kushughulikia mambo yote.

“Nachukua nafasi hii kuwapa pole wananchi wote waliopatwa na haya, Jeshi la Polisi kupitia mipango yake kupitia operesheni na kwa kutanguliza intelejensia tumeshakama watu wengi.”


Mapendekezo ya tume

Katika mkutano wa jana, Waziri Masauni alizungumzia Tume iliyoundwa kuchunguza uhalifu nchini akisema ripoti yake imejaa mapendekezo mengi mazuri kwa ajili ya usalama wa nchini na mojawapo ni suala la kuimarisha mifumo ya usalama kwa ngazi za chini ambayo wameanza kuifanyia kazi.

“Ripoti ile ni nzuri sana, imejaa mambo mazuri na mapendekezo yenye tija, mojawapo ni suala la kuimarisha mifumo ya usalama ngazi ya chini ambayo kwenye kata tumepeleka maofisa lakini taarifa ni kubwa na mapendekezo ni mengi tena mazuri,”alisema.


Kauli ya IGP Wambura

IGP Wambura, alisema wapo watu wengine wanaendelea kujipanga kufanya uhalifu kwa kuwa hawaoni kinachoendelea lakini anaamini wanao ndugu zao wanaosoma magazeti, kuangalia runinga na kufuatilia mitandao hivyo waambie wakae chonjo.

“Jeshi la Polisi haijawahi kushindwa, nawaonya wakae chonjo, kumetokea wahalifu wengi ambao ni wapokeaji wa mali za wizi, hawa nao wakae chonjo kwani bila wao wahalifu wasingeongezeka,”alisema Wambura.

Alibainisha kuwa ni wakati muafaka kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kutoa taarifa sahihi.

“Viongozi wa Serikali za Mitaa waimarishe vikundi vya ulinzi ili viweze kusaidia kwenye ulinzi, wananchi wako salama na wataendelea kuwa salama. Wananchi waendelee na shughuli za uzalishaji mali,”alisema.


Majeruhi wasimulia

Mmoja wa waliovamiwa na kikundi cha uhalifu, Gadi Solomon alisema Februari 11, 2022 saa nne usiku eneo la Chamazi, Songas alivamiwa na vijana watatu waliokuwa kwenye bodaboda wakati akitoka kazini.

Alisema vijana hao wenye umri unaokadiriwa miaka 18 hadi 25 waliificha bodaboda gizani umbali wa mita 50 kisha walianza kumjeruhi kwa mapanga mwilini.

“Sikuwa na wazo kama ni kikundi cha wahalifu, niliwafuata ili kuwapokonya begi walilonichukulia ambalo lilikuwa na simu pamoja na vifaa vingine vya kufanyia kazi. Hata hivyo walifanikiwa kunidhibi ti kwa mapanga. Walinikata vidole viwili vya mkono wa kushoto, kiganja cha mkono wa kulia, paji la uso na magoti kwa sababu walikuwa wameniangusha chini,” alisema Solomon.

Katika tukio lingine lililotokea Jumapili iliyopita Mbagala Maji Matitu, vijana waliokuwa na silaha walivamia nyumba moja saa nane usiku na kumjeruhi Mnyonge Muhidini (28).

Akisimulia tukio hilo Mnyonge alisema alilazimika kuamka baada ya kusikia watu wakirushiana maneno na kugundua walikuwa ni kikundi cha uhalifu wakibishana na askari jamii.

“Yule askari kumbe alikuwa anakuja kutoa taarifa kwetu kwamba wezi wapo nje wanataka kutuvamia kwahiyo wakawa wanakimbizana na kujibizana,”alisema.

“Ghafla nikasikia wanavunja geti na mimi nikatoka sebuleni kwenda chumbani kwangu kuchukua nondo, wakati natoka nikakuta wanamalizia kuvunja mlango wa mbao,alisema Mnyonge na kuongeza,” alisema Mnyonge

Mnyonge alisema wa kwanza alipambana naye na kufanikiwa kumtupa pembeni, wenzake walipoona amezidiwa nguvu waliigia watatu wakiwa na mapanga na kuanza kumshambulia.

“Baada ya kuzidiwa nguvu, vijana hao walichukua runinga ya sebuleni, chumbani na simu janja na kuondoka zao.

Imeandikwa na Fortune Francis, na Elizabeth Edward (Dar); Habel Chidawali (Dodoma)