Polisi yawaachia kina Mbowe kwa dhamana, baadhi wakwama
Muktasari:
- Jeshi la Polisi limesema katika kuzuia kongamano lililokuwa limeandaliwa na Baraza la Vijana Chadema liliwakamata viongozi na wafuasi wa chama hicho na sasa baadhi yao wameachiwa usiku huu.
Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limethibitisha kuwashikilia na kuwahoji viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wapatao 520 na kuwaachia huru baadhi yao kwa dhamana.
Pia limesema ambao hawakuachiwa ni wale walioshindwa kukidhi masharti ya dhamana au kuwa na makosa zaidi ya moja, ikiwemo jinai.
Limesema halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu za nchi kwa kuiga mataifa mengine.
Akizungumza usiku huu Agosti 12, 2024 Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo nchini, Awadhi Haji amesema Agosti 11 walikamatwa 375, ikiwa wanaume 261 na wanawake 114 na leo Agosti 12 wamekamata 145, wanaume 112 na wanawake 33.
"Kati ya watuhumiwa waliokamatwa kwa kosa la kukaidi kuendelea na safari kuja Mbeya, walikuwemo viongozi wakuu wa Chadema waliokamatiwa mkoani hapa eneo la Kadege, ambao ni Makamu Mwenyekiti Tundu Lisu, Katibu Mkuu, John Mnyika, Mwenyekiti wa Kanda, Joseph Mbilinyi 'Sugu', Katibu Mwenezi wa Bavicha Taifa, Twaha Mwaipaya na Makamu Bavicha, Moza Ally.
"Agosti 12 Jeshi la Polisi limewakamata wafuasi wengine 145 wakiwamo viongozi wakuu wa chama hicho Taifa, ambao ni Mwenyekiti Freeman Mbowe na Mwenyekiti Bavicha Taifa, John Pambalu katika Uwanja wa Ndege Songwe wakija kushiriki kongamano lililopigwa marufuku na kufanya jumla ya waliokamatwa kufikia 520" amesema Kamanda Haji.
Kamanda huyo amesema kuwa watuhumiwa wote walihojiwa kisha kurejeshwa maeneo walipotoka kwa kusindikizwa na Polisi, huku waliokamatwa kutoka Mkoa wa Mbeya wakipewa dhamana.
Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika Jiji la Mbeya na maeneo yote nchini penye viashiria vya uvunjifu wa amani na linaendelea kufuatilia mipango ya kufanya uvunjifu wa amani na atakayebainika atachukuliwa hatua bila kujali nafasi wala cheo chake.
"Jeshi la Polisi linawataka viongozi wote wa vyama vya siasa na wafuasi wake kufuata sheria na taratibu za nchi na litachukua hatua kali za kisheria kwa mtu au kikundi kitakachojihusisha na vya uvunjifu wa amani," amesema Kamanda huyo.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi