Amnesty International, TLS na TEF wapaza sauti kukamatwa viongozi Chadema, wanahabari
Muktasari:
- Wimbi la wanaopinga na kulaani vitendo vya kukamatwa kwa viongozi wa Chadema linaendelea kuongezeka, baada ya Shirika la Kimataifa la Haki za Bindamu la Amnesty International kuingilia kati.
Dar es Salaam. Shirika la Kimataifa la Kupigania Haki za Binadamu la Amnesty International, limeungana na wadau wa ndani kulaani kukamatwa kwa viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendele (Chadema).
Matamko ya kulaani vitendo hivyo yameendelea kutolewa na wadau mbalimbali wa haki za binadamu, wakipinga uamuzi wa Jeshi la Polisi Tanzania kuwashikilia viongozi wa Chadema pamoja na waandishi wa habari.
Makundi ya wanaoshikiliwa na jeshi hil, yanahusisha viongozi wa chama hicho, akiwemo mwenyekiti Freeman Mbowe, wanahabari na wadau wengine.
Kushikiliwa kwao kunatokana na uamuzi wao wa kuelekea jijini Mbeya kushiriki maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyopangwa kufanywa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).
Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilishaingilia kati shughuli hiyo na kupiga marufuku isifanyike kwa kile lilichodai vuguvugu la kuvunjwa kwa amani na vurugu ndani yake.
Sambamba na tamko la Amnesty International, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) wamelaani vitendo hivyo.
Katika taarifa yake ya leo Jumatatu, Agosti 12, 2024, shirika hilo la kimataifa limezitaka mamlaka nchini Tanzania kuheshimu, kulinda na kutekeleza haki za binadamu wote kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2025.
“Mamlaka zinapaswa kukomesha ukamataji haramu wa wanasiasa wa upinzani na kuweka vizuizi juu ya haki ya wananchi kujumuika,” imeeleza taarifa ya shirika hilo.
Limekwenda mbali na kutaka wote walioshikiliwa waachiwe huru na kama kuna mwenye hatia mamlaka zinapaswa kuheshima haki zao za kuwaeleza sababu za kuwakamata.
Tamko la TLS
Katika hatua nyingine, TLS kimeungana na wadau wengine kulaani kukamatwa kwa viongozi na wafuasi wa Chadema na wanahabari kulikofanywa na Jeshi la Polisi.
“Jeshi la Polisi pamoja na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa imekuwa na uzito mkubwa katika kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika hasa pale zinapotolewa kauli zenye viashiria vya uhalifu kutoka kwa upande wa viongozi wa Chama Tawala,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ya TLS iliyosainiwa na rais wake, Boniface Mwabukusi imeitaja Ibara ya 18 na 20(1) ya Katiba ya nchi inayotoa haki na uhuru wa watu kujieleza, kukusanyika na kujumuika.
Kadhalika, imeeleza haki hizo zinalindwa kwenye mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeiridhia, hivyo ina wajibu wa kuziheshimu na kuzitekeleza ipasavyo.
“TLS inasikitishwa na ukiukwaji huu wa Katiba na ukamatwaji huu unaoendelea ambao unafifisha uhalisia wa 4Rs za Rais Samia Suluhu Hassan ambazo ni maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya,” imesema.
Chama hicho kimetoa wito na kulisihi Jeshi la Polisi nchini, kuheshimu utawala wa sheria na mara zote lijielekeze katika kulinda raia na mali zao na kuacha kuingilia shughuli za vyama vya siasa ambazo kimsingi zinaongozwa na sheria ya vyama vya siasa.
“Hivyo basi, tunalisihi Jeshi la Polisi kuacha mara moja matendo yenye kuashiria uminyaji wa haki ya kujumuika na kujieleza jambo ambalo ni uvunjwaji wa Katiba na sheria za nchi.
“Tunavitaka vyombo vya usalama hususan Jeshi la Polisi viimarishe uwezo wao wa kulinda makundi haya wakati yanapotaka kutumia haki zao za kikatiba katika shughuli zao kwa mujibu wa taratibu na sheria zetu, na watambue kwamba wajibu wao ni kutoa ulinzi na kama kuna viashiria vya uhalifu wavidhibiti na si kuzuia vyama au makundia kiraia kujumuika kwasababu za kiujumla zisizo na maelezo yanayojitosheleza,” kimeeleza chama hicho.
Imeeleza chama hicho kupitia kamati maalumu ya mawakili kimeelekeza kufanyika tathmini na kuchukuliwa kwa hatua stahiki za kisheria kwa kila ofisa aliyehusika kusababisha kadhia hiyo kwa jina lake na kuhakikisha utii na uzingatiwaji wa matumizi bora ya madaraka katika Ofisi za Umma.
TEF: Tusiruhusu kurudi gizani
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa taarifa likitaka waandishi wa habari watatu waliokuwa nje ya ofisi za Chadema jijini Mbeya wakisubiri kufanya mahojiano na viongozi wa chama hicho waliokuwa wanaendelea na kikao cha ndani ofisini kisha kukamatwa, waachiwe.
Taarifa ya TEF iliyotolewa na mwenyekiti wake, Deodatus Balile imewataja waandishi hao ni, Ramadhan Hamis, Fadhili Kirundwa wa Jambo TV pamoja na Francis Simba ambaye ni Mpiga Picha wa Chanzo TV.
Balile amesema Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), inatoa haki ya watu kukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa bila kujali mipaka ya nchi. Sambamba na Katiba, Kifungu cha 7(1)(a)(b) na (c) cha Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kama ilivyorekebishwa Mwaka 2023, kinatoa haki kwa waandishi wa habari kufanya kazi ya uandishi wa habari.
Amesema ni jukumu la waandishi wa habari kuhabarisha umma juu ya kila jambo linaloendelea, hivyo mwandishi hapaswi kukamatwa au kuadhibiwa kwa kufanya kazi hii.
Balile amesema Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) pamoja na kuendelea na mawasiliano na viongozi na taasisi mbalimbali, wanavisihi vyombo vya dola kuwaachia mara moja waandishi hao na bila masharti, kwa sababu kuwapo kwao katika eneo la tukio, wanaamini walikuwa wanafanya kazi na si sehemu ya siasa au chochote kilichokuwa kinaendelea.
“Tunalaani matukio ya kukamata waandishi wa habari. Matukio haya yanaharibu heshima kubwa ya Tanzania katika kulinda Uhuru wa Vyombo vya Habari aliyoijenga Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021 kwa kurejesha uhusiano mzuri na vyombo vya habari. Sisi Jukwaa la Wahariri Tanzania, tusingependa kuona Tanzania ikirejea katika enzi za giza za kamatakamata. Tunasema waandishi waliokamatwa waachiwe haraka,” amesema.