Polisi yazuia maandamano ya ACT-Wazalendo, wajipanga tena

Polisi wakipambana kuwazuia vijana wa ACT-Wazalendo nje kidogo ya ya Makao Makuu ya Chama hicho leo Jumanne Aprili 18 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga.

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT-Wazalendo, Abdul Nondo ameeleza sababu ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano, na kuahidi kujipanga tena kumuona Rais.

Dar es Salaam. Wakati maandamano ya Ngome ya Vijana wa ACT-Walendo yakishindwa kufanyika, Mwenyekiti wa Ngome hiyo Abdul Nondo amesema wanajipanga kufanya maandamano siku nyingine.

 Nondo amesema maandamano hayo ya amani yalipangwa kuanzia Manzese hadi Ikulu kuonana na Rais Samia Suluhu Hasaan na kumfikishia ujumbe wa kutokukubaliana na ubadhilifu wa fedha za umma uliofanywa, kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ya kila mwaka.

Aprili 5 Mwaka huu, (CAG), Charles Kichele aliwasilisha ripoti yake mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan ikionyesha ubadhilifu wa mali za umma kiasi cha kuwaibua wananchi wanaotaka hatua stahiki zichukuliwe.

Nondo ameeleza hayo Jumanne Aprili 18, 2023 muda mfupi baada ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano yaliyokuwa yaanzie kwenye ofisi za makao makuu zilizopo Magomeni.

Nondo amesema kwenye kikao kile Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) aliwaambia yeye ana mawazo tofauti na maandamano hayo, kwani wanaona hatua stahiki zimeanza kuchukuliwa.

“Baada yakutueleza hivyo sisi tulimjibu RPC bado hatua stahiki hazijachukuliwa, akatupa barua ikipiga marufuku maandamano hayo lakini sisi tukasema ni lazima tuandamane kwa kuwa ni maandamano ya amani.

Mwenyekiti huyo amesema awali maandamano hayo yalipangwa kuanzia Manzese lakini baada ya Polisi kuanza kuzunguka tangu alfajiri wakaona waanzie kwenye ofisi za chama hicho hata hivyo polisi waliwazuia.

 "Tunaenda kujifungia kuangalia ni namna gani yakufanya tena maandamano haya, hadi kumfikia Rais, risala hii tuliyokuwa tumpelekee ntaisoma hadharani ili kila mtu ajue ujumbe tuliokuwa tunampelekea." Amesema.


Hali ilivyokuwa

Wakati vijana hao wanataka kuanza maandamano ilifika gari moja ya polisi iliyosimama mita chache kutoka zilipo ofisi hizo na walipokaribia kutoka nje wakiwa na mabango alifika askari mmoja na kuwazuia kutoka.

Kufuatia hali hiyo, Polisi waliongezeka wakiwazuia wasitoke nje na wakitaka kumkamata mwenyekiti wa Ngome hiyo kutokana na msimamo wake wake kubishana na maafisa hao wa Polisi akiwataka waachwe wafanye maandamano.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondo, Mtatiro Kitinkwi ili kutolea ufafanuzi simu yake iliita bila kupokelewa huku Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Muliro Jumanne akisema atafutwe baadae.