Precision yaanza mchakato ulipaji fidia

Mkurugenzi wa kampuni ya Precision Air, Patrick Mwanri akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Biashara wa kampuni hiyo, Lilian Masawe. Picha na Elizabeth Edward

Muktasari:

  • Wakati Baraza la Mawaziri likitoa maelekezo kwa wataalamu wa ndani kushirikiana na wa nje kufanya uchunguzi kuhusu ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air na kuagiza vitengo vinavyohusika na kukabiliana na majanga kuimarishwa, shirika hilo limeanza mchakato wa kuwezesha malipo ya fidia kwa familia zilizoathiriwa na ajali hiyo.

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Mawaziri likitoa maelekezo kwa wataalamu wa ndani kushirikiana na wa nje kufanya uchunguzi kuhusu ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air na kuagiza vitengo vinavyohusika na kukabiliana na majanga kuimarishwa, shirika hilo limeanza mchakato wa kuwezesha malipo ya fidia kwa familia zilizoathiriwa na ajali hiyo.

Ajali hiyo ilitokea Novemba 6 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 19 na wengine 24 kunusurika, baada ya ndege namba kuanguka katika Ziwa Victoria jirani na Uwanja wa Ndege wa Bukoba.

Juzi, Mkurugenzi wa Precision Air, Patrick Mwanri akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema tayari wameanza mchakato utakaowezesha waathirika kupata fidia ambayo inatokana na bima ya ndege iliyopata ajali.

Mwanri alisema mchakato huo utakuwa kati ya familia za waathirika na kampuni hiyo, hivyo utakuwa wa siri baina ya pande hizo na utafanyika kwa umakini mkubwa.

“Shirika letu lina bima na ipo kulingana na taratibu za uendeshaji wa mashirika ya ndege. Hivi ninavyoongea taratibu zile zimeshaanza na wahusika tumeshaanza kuwasiliana nao ili waweze kupata taarifa rasmi ya nini kinahitajika,” alisema.

“Mara nyingi suala hili hufanyika kwa faragha kati ya wahusika na sisi hatutalileta hadharani. Tuna mawasiliano ya karibu na majeruhi wote tangu wakiwa hospitali hata baada kutoka tukiwasaidia kwa namna mbalimbali kadiri ya uwezo wetu,” alisisitiza.

Licha ya mkurugenzi huyo kutoweka wazi kiasi ambacho waathirika watalipwa, hivi karibuni Mwenyekiti wa Chama cha Kampuni za Bima, Khamis Suleiman alilieleza gazeti hili kuwa wanaweza kupokea takribani Dola 129,000 za Marekani (sawa na Sh300 milioni) kila mmoja ikiwa watafuata utaratibu unaofaa wa fidia, kwa mujibu wa kanuni bora za kimataifa zinazoongoza sekta ya usafiri wa anga.

Alisema kiasi hicho kinaweza kuongezeka, kama waathirika watakuwa huru kwenda mahakamani kudai fidia kulingana na kiwango cha uharibifu, ambao wanaweza kudai katika mchakato huo.

“Kwa sheria za uwajibikaji, kama ilivyoelezwa kwenye mikataba ya usafiri wa anga, mtu anatakiwa kulipwa Dola 129,000... Ndugu zao watakuwa huru kuomba malipo kulingana na kiwango cha madhara kama yatakavyothibitishwa na mamlaka husika,” alisema Suleiman.

Pia, alisema kwa kuwa mfumo wa kuwekea bima ndege kwa kiasi kikubwa unatokana na utaratibu wa kurudisha bima kati ya kampuni ya bima ya ndani na ile ya nje, mapato ya ajali hiyo yatabaki ndani ya nchi.

Mwananchi ilimtafuta Luga Biteya, kaka wa ndugu wawili Aneth na Atulinda waliopoteza maisha katika ajali hiyo ambaye alieleza kuwa bado hawajapata taarifa za mchakato huo.

“Kiukweli hatujasikia chochote, huenda wameanza kwa watu wengine ila hata sisi tunasubiri kusikia kwao na tunajaribu kuwa na vitu ambavyo vinaweza kuhitajika mfano cheti cha kifo,” alisema Biteya huku akishukuru Serikali na wadau wa sekta ya anga kwa ushirikiano wao.