Profesa Kabudi azushiwa jambo, Dk Mwakyembe asema uamuzi ulikuwa wa mawaziri wote

Muktasari:

  • Kutajwa kwa jina la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Profesa Palamagamba Kabudi kumezua utata na mabishano bungeni, huku Serikali ikisema asilaumiwe peke yake.

Dodoma. Kutajwa kwa jina la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Profesa Palamagamba Kabudi kumezua utata na mabishano bungeni, huku Serikali ikisema asilaumiwe peke yake.

Akizungumza  katika chombo hicho cha kutunga sheria leo Ijumaa Mei 17, 2019, mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alimtaka Profesa Kabudi  kujiuzulu au kuwajibishwa kwa maelezo kuwa alishauri kampuni ya Indo Power ya Kenya inunue korosho nchini wakati haikuwa na uwezo.

"Tunampongeza Rais (John Magufuli) kwa kuchagua wasomi, lakini tuliamini Profesa (Kabudi) angeweza kuwa na uelewa mpana wa kumshauri Rais na Taifa lakini ametuingiza chaka, lazima aachie ngazi," amesema Msigwa.

Kaimu kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni, Dk Harrison Mwakyembe alimtetea waziri huyo kwamba uamuzi huo (wa kampuni hiyo kukubaliwa kununua korosho) haukuwa wake peke yake, akisisitiza kuwa ulikuwa wa mawaziri wote

Dk Mwakyembe ambaye ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema mawaziri wanawajibika pamoja hivyo jambo lolote linalotendeka ni kwa mashirikiano ya pamoja.

"Mheshimiwa mwenyekiti (wa Bunge), sisi tunafanya kazi kwa pamoja lakini wenzetu wanapiga kelele pamoja, siyo sahihi kumlaumu mtu kwani hakusimama mezani na kuamua peke yake," amesema Mwakyembe.

Baada ya kauli hiyo ilizuka kelele kwa wabunge wa pande zote na naibu Waziri wa Viwanda, Stella Manyanya alisimama na kusema Serikali inazo taarifa kuwa baadhi ya wabunge walikuwa wanaomba rushwa kutoka kwa kampuni na wanazifanyia kazi ili wakati mwingine wawataje.

"Humu ndani Serikali inazo taarifa kuwa baadhi ya wenzetu huko (anaonyesha kidole upande walioketi wabunge wa  upinzani) walikuwa wanaomba rushwa kwa kampuni tunachunguza na tutawataja," amesema Manyanya.

Mwenyekiti wa Bunge,  Andrew Chenge amewatuliza wabunge kwa kutishia kuwatoa wengine nje baada ya wabunge wa upinzani kutaka Manyanya afute kauli yake hiyo.