Profesa Kitila alivyoichambua Dira 2050
Muktasari:
- Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji imetaja malengo mahususi, shabaha, misingi mikuu , vichocheo vitano vinavyoweza kurahisisha mageuzi ya uchumi katika Dira 2050.
Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema malengo mahususi ya Dira 2050 ni kuifanya Tanzania ifikie hadhi ya uchumi wa kipato cha ngazi ya juu.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB), uchumi wa kati ngazi ya juu ni uchumi ambao pato la Taifa kwa mtu mmoja lina thamani ya Dola za Marekani kati ya 4,516 na 14,005.
Profesa Kitila amesema hayo leo, Alhamisi, Julai 17, 2025, wakati wa uzinduzi wa Dira 2050 unaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema dira hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia maeneo saba, lengo kuu (mwelekeo), misingi mitano ya Dira 2050, malengo manne, shabaha 18, msingi mkuu wa Dira 2050, nguzo tatu za Dira 2050, vichocheo vitano vya utekelezaji wa Dira 2050, na sekta tisa za kimageuzi.
Amesema lengo kuu au mwelekeo wa dira ni kuwa na Taifa jumuishi, lenye ustawi, haki na linalojitegemea.
Ametaja misingi mitano itakayoongoza dira kuwa ni kudumisha demokrasia, haki na uhuru, utu, amani na umoja, kulinda mazingira na matumizi endelevu ya utajiri na rasilimali za asili na kudumisha utamaduni na maadili ya Taifa.
Malengo mahususi ya dira ni kuifanya Tanzania kufikia hadhi ya uchumi wa kipato cha ngazi ya juu, ambapo kwa mujibu wa Benki ya Dunia, uchumi wa kati ngazi ya juu ni ule ambao pato la Taifa kwa mtu mmoja lina thamani ya dola za Marekani kati ya 4,516 na 14,005.
Profesa Kitila amesema malengo mengine ni maisha bora na ustawi kwa wote, Taifa linalohifadhi na kutumia rasilimali za asili kwa ufanisi, uendelevu na tija na linalostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Pia, kuwa na jamii yenye umahiri na ujuzi wa kutumia teknolojia za kidijitali katika kuchochea ubunifu na kuongeza ushindani wake kimataifa.
Shabaha za Dira 2050
Profesa Kitila amesema shabaha ya dira ni Tanzania kuwa na pato la Taifa lenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja lenye thamani ya dola za Marekani 7,000 kwa mwaka.
Amefafanua kuwa, kwa thamani ya leo, dola za Marekani 7,000 ni sawa na Sh18.2 milioni kwa mwaka au Sh50,556 kwa siku, kutoka dola 1,277 kwa mwaka (Sh3.32 milioni), Sh276,688 kwa mwezi au Sh9,233 kwa siku kwa sasa.
Pia, shabaha nyingine ni kutokomeza umaskini uliokithiri kwa makundi yote ya jamii.
Ametaja shabaha nyingine kuwa ni kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika na miongoni mwa nchi 10 bora duniani, na Mtanzania kuishi wastani wa miaka 75 yenye afya na furaha kutoka miaka 68 ya sasa.
Nyingine ni watoto wote wa kike na wa kiume kuwa na fursa sawa ya malezi bora ya utotoni, huku angalau asilimia 90 ya watoto wote wakiwa katika hatua sahihi za ukuaji unaoonesha uwezo wao kamili ifikapo umri wa miaka mitano.
Pia, kutokomeza vifo vya wajawazito, watoto wachanga na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, huduma bora za afya kwa wote na mfumo bora na jumuishi wa elimu na mafunzo katika ngazi zote.
“Watoto wote wa kike na wa kiume wana fursa sawa za kupata elimu ya awali yenye kujenga msingi imara kwa ajili ya kujifunza na kujielimisha bila ukomo,” amesema.
Shabaha nyingine ni Watanzania wote kupata elimu msingi bora (miaka sita ya elimu ya msingi na miaka minne ya sekondari) na angalau asilimia 25 kupata elimu ya juu.
Nyingine ni upatikanaji wa huduma jumuishi za hifadhi ya jamii kwa wote, upatikanaji sawia wa maji safi na salama, huduma za usafi wa mazingira na nishati safi, pamoja na angalau asilimia 50 ya Watanzania kuwa na ajira zenye staha katika sekta rasmi.
Pia, kuwa na viwango vya juu vya uhifadhi wa mazingira na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, na kuifanya Tanzania kuwa kati ya nchi 10 bora barani Afrika na jamii yenye umahiri wa kidijitali, ambapo asilimia 70 ya wananchi wanakuwa na ujuzi wa Tehama.
Ametaja shabaha nyingine kuwa ni zaidi ya asilimia 80 ya huduma za Serikali kutolewa kwa njia ya kidijitali, hivyo kuwezesha wananchi wote kupata huduma za msingi kwa urahisi.
Pia, kuongezeka kwa matumizi ya nishati ya umeme kufikia wastani wa 3,000 kWh kwa kila mtu kwa mwaka, na Tanzania kuwa kinara barani Afrika na miongoni mwa nchi 10 bora duniani katika kupunguza pengo la kijinsia kwa angalau asilimia 85.
Misingi mikuu
Kwa upande wa misingi mikuu, Profesa Kitila amesema ni utawala, amani, usalama na utulivu.
Dira 2050 imesimikwa katika misingi mikuu ya uchumi imara, jumuishi na shindani, uwezo wa watu na maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Amevitaja vichocheo vinavyoweza kurahisisha mageuzi ya kiuchumi ili kufikia shabaha ya uchumi wa ngazi ya juu kuwa ni usafirishaji fungamanishi, nishati, sayansi na teknolojia, utafiti na maendeleo, na mageuzi ya kidijitali.
Utekelezaji
Profesa Kitila amesema kuwa katika kujiandaa na utekelezaji wa Dira 2050, na kwa kuzingatia maelekezo ya Rais Samia, Tume ya Taifa ya Mipango inaendelea kuchukua hatua za kuandaa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu (LTPP).
Amesema huo ndio utakuwa mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa Dira 2050.
Pia, amesema hatua nyingine ni kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP) ambao utatafsiri maono ya Dira 2050 katika kipindi cha miaka mitano, na utakamilika kabla ya Novemba 2025 ili upelekwe bungeni.
Ushiriki wa wananchi
Profesa Kitila amesema watu milioni 1.13, sawa na asilimia 81 waliojitokeza kutoa maoni yao kwa njia ya ujumbe wa simu (USSD), tovuti na mitandao ya kijamii walikuwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 35.
Amesema hiyo inaakisi demografia ya Tanzania, ambapo asilimia 76 ya watu wapo chini ya umri wa miaka 36.
Amesema pia kuwa, ili kuhakikisha maoni na sauti za wananchi zinaratibiwa na kuakisiwa kikamilifu katika maudhui ya Dira 2050, asasi za kiraia (Azaki) kupitia uratibu wa taasisi ya Foundation for Civil Society (FCS) walipewa nafasi maalumu ya kupitia maudhui ya rasimu ya Dira 2050.
Amesema waliifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa baada ya kujifungia na timu yao kwa wiki kadhaa.
Aidha, amesema kuwa ili kuhakikisha maudhui ya Dira 2050 yanakuwa jumuishi na yanazingatia masuala muhimu ya usawa wa kijinsia, viongozi na wanachama wa mtandao wa jinsia nchini walipewa nafasi maalumu ya kupitia maudhui ya rasimu na kutoa maoni yao ya jumla na mahsusi.
Amesema walikusanya pia maoni ya viongozi wakuu waliopo madarakani na waliostaafu, ambapo walipata maoni na maelekezo ya viongozi 44.
Pia, amesema walikutana na viongozi 19 wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa, katika vikao viwili tofauti, Mei 27, 2024 na Desemba 14, 2024.
“Baada ya kupitia rasimu ya dira na kutoa maoni yao, viongozi wa vyama vya siasa walikubaliana kwa kauli moja kuwa ilani za vyama kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 zizingatie na kuakisi maudhui ya Dira 2050,” amesema.
Yanayoingia kwenye historia
Aprili 3, 2023, jijini Dodoma, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, alizindua rasmi mchakato wa maandalizi ya Dira 2050.
Desemba 9, 2023, jijini Dodoma, Rais Samia alizindua rasmi nyenzo na mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na wadau kuhusu maudhui ya Dira 2050.
Pia alizindua timu kuu ya kitaalam ya kuandaa Dira 2050.
Desemba 11, 2024, Zanzibar, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, alizindua rasmi rasimu ya Dira na awamu ya pili ya kukusanya maoni ya uhakiki kutoka kwa wadau.
Machi mosi, 2025, jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Maandalizi ya Dira 2050 alimkabidhi rasmi Waziri wa Nchi – Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, rasimu ya dira tayari kuingia katika mchakato wa maamuzi ndani ya vyombo vya Serikali.
Juni 22, 2025, jijini Dar es Salaam, Baraza la Mawaziri liliidhinisha rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuipa jina Dira 2050, ambalo litatumika kwa lugha zote, Kiswahili na Kiingereza.