Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Maghembe awekewa pingamizi

Waziri wa Maji Prof,Jumanne Maghembe .

Muktasari:

Mkoani Kilimanjaro, mgombea wa Chadema, Henry Kileo amemwekea pingamizi mgombea wa NCCR-Mageuzi, Youngsaviour Msuya pamoja na mgombea wa CCM.

Mwanga. Wakati kampeni zikianza, wagombea mbalimbali wamewekewa pingamizi huku baadhi ya majina yakipita bila kupingwa kwa vyama mbalimbali.

Mkoani Kilimanjaro, mgombea wa Chadema, Henry Kileo amemwekea pingamizi mgombea wa NCCR-Mageuzi, Youngsaviour Msuya pamoja na mgombea wa CCM.

Mgombea wa CCM aliyewekewa pingamizi lenye sababu nne ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe anayegombea ubunge kwa kipindi cha nne mfululizo.

Katika pingamizi lake, Kileo amedai kuwa Profesa Maghembe aliapa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo badala ya Hakimu wa wilaya pia ameambatanisha picha ambayo haijapigwa ndani ya miezi mitatu.

Pia, anadai kuwa Profesa Maghembe hakuambatanisha risiti ya malipo ya tamko rasmi na fomu yake imegongwa muhuri wa katibu wa wilaya wa CCM badala ya ofisi ya CCM Wilaya ya Mwanga.

Kwa upande wa mgombea wa NCCR-Mageuzi, Kileo anadai kuwa fomu za mgombea huyo zimegongwa muhuri wa katibu wa Wilaya ya Mwanga badala ya wa ofisi ya wilaya.

Halikadhalika anadai mgombea huyo amekwenda kuapa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Moshi badala ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mwanga.

Kigoma

Baadhi ya Wagombea wa CCM katika Majimbo ya Kasulu mjini na Kigoma kusini wamewekewa pingamizi kutokana na kile kinachodaiwa ni kujaza fomu za kuomba kuteuliwa na Tume kimakosa, hivyo kupoteza sifa za kuwa wagombea.

Mgombea wa CCM katika Jimbo la Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko (CCM) amewekewa pingamizi na mgombea wa ACT-Wazalendo, Moses Machali kutokana na mgombea huyo kujaza fomu yake akionyesha kwamba alizaliwa Agosti 15, 2015 ikimaanisha kwamba hadi alipokabidhi fomu kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo alikuwa na umri wa siku sita.

“Nimeweka pingamizi baada ya kubaini kosa katika fomu ya mgombea wa CCM (Daniel Nsanzugwanko) aliyedai amezaliwa Agosti 15, 2015. Kwa mujibu wa sheria za Uchaguzi, mgombea anapaswa kuwa na umri usiopungua miaka 21, sasa Nsanzugwanko amekula kiapo mbele ya Mahakama akionyesha kuwa ana umri wa siku sita, hivyo hana sifa za kuteuliwa kuwa mgombea,” alisema Machali.

Kwa upande wake Nsanzugwanko alipopigiwa simu ili atoe ufafanuzi wa sakata hilo alipokea kwa sekunde nne bila kuzungumza kitu na baadaye aliikata na aliandika ujumbe mfupi wa maneno kwamba, “Niletee meseji...” hata hivyo katika majibu aliyotoa baada ya kusoma ujumbe huo, alijibu kuwa: “Haiwezi kuniondoa kugombea kaka. Pingamizi hilo halina nguvu.”

Pia, tamko la kiapo katika fomu iliyojazwa na Nsanzugwanko inaonyesha kuwa ilijazwa Agosti 19, 2015 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu, Janeth Mtega akithibitisha kwamba maelezo aliyojaza ni sahihi.

Katika Jimbo la Kigoma Kusini pia hali siyo shwari baada ya mgombea wa NCCR-Mageuzi, David Kafulila kuweka pingamizi akipinga uteuzi wa mgombea wa CCM, Hasna Mwilima kwa madai ya kutumia majina matatu tofauti katika fomu zake za uteuzi.

Anadai kuwa sehemu moja ya fomu inaonyesha anagombea kupitia chama chenye jina la “Mapinduzi (CCM)” huku ikidaiwa hakuna chama kilichosajiliwa kwa jina hilo.

Katika barua yake ya pingamizi kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kigoma Kusini, Reuben Mfune, Kafulila anadai fomu namba 8B yenye maelezo binafsi ya mgombea, Mwilima ametumia jina la Hasna Sudi Katunda Mwilima, wakati kwenye tamko la wadhamini ametumia jina la Hasna Mwilima.

Katibu wa CCM Wilaya ya Uvinza, Mohamed Gwama alisema pingamizi hilo siyo la msingi na kudai kwamba aliyeweka pingamizi hilo anatapatapa baada ya kubaini nguvu ya CCM kuwa ni kubwa jimboni humo.

“Fomu za mgombea wetu (Hasna Mwilima) zipo sahihi, hili linalotokea hapa ni dalili ya NCCR Mageuzi kukata tamaa ya ushindi,” alisema.

Mwilima alikiri kuwekewa pingamizi na Kafulila huku akidai kwamba hoja zilizotolewa dhidi yake hazina msingi.

Mwanza

Wagombea saba kati ya 10 waliojitokeza kugombea Jimbo la Nyamagana wamepitishwa kuwania nafasi hiyo huku watatu wakishindwa kurudisha fomu.

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Halifa Hida jana alisema wagombea watatu wameshindwa kupitishwa kwa madai kuwa walichelewa kurudisha fomu baada ya muda kumalizika.

Walioteuliwa ni Faida Potea (CUF), Chacha Okong’o (ACT).Mohamed Msanya (Jahazi Asilia), Ramadhan Mtoro (UDP), Ahmad Mkangwa (NRA), Stanslaus Mabula (CCM) na Ezekiah Wenje (Chadema).

“Walioshindwa kurejesha fomu wako watatu, Saenda Emmanuel (UPDP), Mwaijumba Mbuli (TLP) na Simba Robert (TADEA), hivyo hawa hawatahusika na shughuli zozote za kampeni kwa mujibu wa sheria, utaratibu na miongozo ya uchaguzi,” alisema Hida.

Mbeya

Vyama vitano vimepitisha majina ya wagombea wa majimbo mbalimbali.

Mbeya Mjini

Waliopitishwa ni Sambwee Shitambala (CCM), Joseph Mbilinyi (Chadema), Mary Komba (Chausta), Tumaini Mwanyalu (Chama cha Demokrasia Makini) na Lusekelo Asheli wa ACT- Wazalendo.

Naye Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ileje, Mussa Otieno aliwataja waliorudisha fomu kuwa ni Janeth Mbene (CCM) Emmanuel Mbuba (NCCR-Mageuzi) na Nuru Mwaji wa ACT-Wazalendo.

Walioteuliwa Jimbo la Rungwe ni John Mwambigija (Chadema), Frank Magoba (ACT-Wazalendo), Saul Amon (CCM), Freddy Mwandemele (UDP) na Nicodemus Ngwalla kupitia DP.

Walioteuliwa Jimbo la Songwe ni Philipo Mulugo wa CCM, Mpoki Mwankusye (Chadema) na Michael Milawila (ACT- Wazalendo).

Jimbo la Lupa ni Njelu Kasaka (Chadema), Mohamed Miraji (ACT-Wazalendo) na Victor Mwambalaswa (CCM).

Jimbo la Mbeya Vijijini ni Oran Njeza (CCM), Zella Abraham (Chadema) na Bariki Mwanyalu wa Chama cha Demokrasia Makini.

Jimbo la Mbozi ni Julius Philipo (ACT-Wazalendo), Godfrey Zambi (CCM) na Pascal Haonga wa Chadema.

Jimbo la Vwawa ni Japhet Hasunga (CCM), Rose Mwashambwe (ACT-Wazalendo) na Phanuel Mkisi (Chadema).

Handeni

Mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Jimbo la Handeni Mjini, Dk Abdallah Kigoda amewawekea pingamizi wagombea wenzake wa vyama vya AFP, Chadema, ADC, TLP na CUF huku mgombea wa Chadema, Saudi Lussewa akimuwekea pingamizi Dk Kigoda.

Msimamizi wa Uchaguzi jimbo hilo, Kenneth Haule alisema pingamizi zote zinafanyiwa kazi.

Msimamizi atupa pingamizi dhidi ya Bashe

Mgombea ubunge kwa tiketi ya CUF Jimbo la Nzega Mjini, Mezza John amemuwekea pingamizi mgombea wa CCM wa jimbo hilo, Hussein Bashe kuwa hakutoa tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi ya mwaka 2015.

Msimamizi wa uchaguzi wa jimboni humo, Hawa Mninga akizungumza na waandishi wa habari jana alisema ametupilia mbali pingamizi hilo kutokana na mgombea huyo kujaza fomu ya tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi ya mwaka 2015.

Hawa alisema mgombea huyo kama wagombea wengine, ametekeleza mahitaji yote yanayopaswa mgombea ayatekeleze ili aweze kukidhi mahitaji halisi na kuongeza kuwa, hakuna sababu ya kumtaka mgombea huyo kujaza fomu kwani ametimiza sifa za kuwa mgombea.

Imeandikwa na Anthony Kayanda, Daniel Mjema, Lauden Mwambona, Mary Mwaisenye na Jesse Mikofu.