Profesa Mkenda alia nyani kuhatarisha usalama wa watoto Rombo
Muktasari:
Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda amesema bado wilaya ya Rombo inakabiliwa na changamoto kubwa ya nyani ambao wamekuwa wakihatarisha usalama wa watoto pamoja na kuharibu mali ikiwemo mazao.
Rombo. Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda amesema bado wilaya ya Rombo inakabiliwa na changamoto kubwa ya nyani ambao wamekuwa wakihatarisha usalama wa watoto pamoja na kuharibu mali ikiwemo mazao.
Amesema maeneo mengi ambayo yameathirika na nyani hao ni maeneo ya kanda za juu ambapo amesema tayari ameshawasiliana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro ambapo amemuahidi kwenda Rombo kuongeza nguvu ya kukabiliana na ongezeko la nyani hao.
Profesa Mkenda ameyasema hayo leo Novemba 15, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhudhuria semina ya watendaji wa vijiji, kata pamoja makatibu wa Mashina wa chama cha Mapinduzi (CCM) iliyokuwa ikitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai pamoja na kamati ya usalama ya mkoa huo.
"Changamoto ya nyani Rombo bado ipo na haijaisha, alikuja Waziri wa Maliasili na timu yake kujaribu lakini bado wapo, hali ya ukanda wa juu ni mbaya vyakula mashambani vimeharibiwa na usalama wa watoto sio mzuri sana,"amesema Profesa Mkenda na kuongeza
"Nimeongea na Waziri wa Maliasili na Utalii akaniambia ataongeza nguvu kwa ajili ya kupambana na nyani hawa, kwasababu hawa nyani wapo kwa ajili ya binadamu na sio binadamu kwa ajili ya wanyama ,"amesema Profesa Mkenda
"Hatuwezi kukubali wanyama wavuke kutoka hifadhini na kuja mtaani kubughudhi wananchi,hivyo Waziri amenihakikishia watakuja kumaliza hili tatizo,"amesema Waziri Mkenda