Profesa Mkenda awaonya wanaCCM Rombo, awakumbusha ya Mramba

Muktasari:

  • Basil Mramba aliwahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kuanzia mwaka 1980 na kudumu katika nafasi hiyo kwa miaka 20 hadi mwaka 2000 ambapo hakufanikiwa kuchaguliwa tena na wananchi, na nafasi yake wakati huo ilichukuliwa na Justin Salakana ambaye alikaa kwa kipindi kimoja cha miaka mitano pekee.

Rombo. Mbunge wa Rombo (CCM) ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amewaomba wananchi wa Rombo, mkoani Kilimanjaro kutofanya makosa kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao katika jimbo hilo,  kama walivyofanya kwa aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, Basil Mramba.

Profesa Mkenda ametoa ombi hilo leo Aprili 21, 2024 kwenye mkutano wa wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Rombo, waliokuwa  wakijadili mambo mbalimbali ya kichama.

Mramba aliwahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kuanzia mwaka 1980 na kudumu katika nafasi hiyo kwa miaka 20 hadi mwaka 2000 ambapo hakufanikiwa kuchaguliwa tena, na wananchi na nafasi yake wakati huo ilichukuliwa na Justin Salakana ambaye alikaa kwa kipindi kimoja cha miaka mitano pekee.

Baadaye mwaka 2005, Mramba alirejea tena kwenye nafasi hiyo ya ubunge baada ya makada wa CCM na wananchi wa wilaya hiyo mkoani Mbeya alikokuwa mkuu wa mkoa, kumwomba arudi kugombea tena katika jimbo hilo, ambapo alikaa kwa kipindi kimoja  na kufuatiwa na Joseph Selasini wa Chadema kati ya mwaka 2010 hadi 2020.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Profesa Mkenda amesema ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2020 zimetekelezwa kwa asilimia kubwa ikiwemo kuanza kwa ujenzi wa kilomita 10 barabara ya Lower Road kwa kiwango cha lami.

Amesema baadhi ya wananchi na makada wa chama hicho walimzushia maneno ya uchonganishi kwamba Mramba alikuwa ni mtu wa kupenda kukaa na matajiri wakati wote, jambo ambalo amesema lilikuwa ni la uzushi na kuchafuana kisiasa.

“Wakati tunagombea, tulisema ilani ya CCM imesema barabara ya Lower Road, ikifika 2025 itafanyiwa upembuzi yakinifu, nikawaambia nichagueni tulete maendeleo, nitaunguruma kama Ngalai (aliyewahi kuwa mbunge wa Rombo), nitatembea kwa uhusiano kama Mramba, upembuzi yakinifu ufanywe haraka, barabara iwekwe lami na kazi imeanza,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema tayari Serikali imetangaza zabuni ya kilomita 10 na mafanikio hayo ni kwa miaka mitatu tangu achaguliwe,  na kuwa yajayo yanafurahisha.

“Kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa msifanye makosa, mnajua wakati Mramba aliposhindwa ubunge Rombo, baadaye watu walienda na jani la 'sale' akiwa mkuu wa mkoa wa Mbeya, kwamba baada ya ile miaka 10, wananchi waligundua  wamekosea.

“Mramba akawaambia mtaenda kunidhalilisha tena, akakubali, akarudi akagombea akapata ubunge, barabara ya Rombo ikapigwa lami na baadaye akaingia kupambana na changamoto ya maji,” amesema waziri huyo.

Pamoja na mambo mengine, Profesa Mkenda amesema Mramba alifanya mambo makubwa akiwa mbunge wa jimbo hilo, ikiwemo kuunganisha mtandao mkubwa wa barabara kwa kiwango cha lami ambapo wananchi wa wilayani hiyo wanamkumbuka nayo.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM wilaya ya Rombo, Mary Shule amewaonya makada wa chama hicho kuacha mara moja tabia ya kuwachonganisha viongozi ndani ya chama hicho kwa kile alichodai wanaweza kuleta mpasuko.

“Tuendelee kukiimarisha chama chetu, tuache malalamiko, tuache tabia ya kuchonganisha viongozi ndani ya chama, tuache tabia hiyo mara moja, vinginevyo tutajikuta tumegawanyika vipande vipande, tutaenda kwenye uchaguzi hatuko wamoja na madhara ya kutokuwa wamoja ni kwenda kushindwa, sasa kama wewe ni mchonganishi, mtoa habari za uongo, acha,” amesema.

Diwani wa kata ya Kingachi, Nestory Ngowi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa  kuleta maendeleo mbalimbali katika kata hiyo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule, vyoo na madarasa yenye thamani ya zaidi ya Sh34 milioni na ukarabati wa miundombinu ya barabara iliyogharimu zaidi ya Sh500 milioni.