VIDEO: Kauli ya Profesa Mkenda mauaji mwanamke Rombo
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Kilimanjaro wakati akitoa ufafanuzi wa taarifa iliyosambaa mtandaoni kuhusu mauaji ya Beatrice Minja, mkazi wa Rombo, Mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Waziri Mkenda amesema taarifa zinazosambaa kwenye mitandaoni kuwa mtuhumiwa Lucas Tarimo anayedaiwa kumchoma visu mara 25 Beatrice Minja hakuwahi kuwa mfanyakazi wake.
Moshi/Mtwara. Wakati taarifa za shambulio lililosababisha mauaji ya mwanamke mkazi wa Rombo, Beatrice Minja, zikiibuliwa mitandaoni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amekanusha kuhusishwa na mtuhumiwa wa kosa hilo.
Beatrice Minja alifariki juzi Desemba 27, 2023 akiwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), hospitali ya Rufaa ya KCMC, alipokuwa akiuguza majeraha yanayodaiwa kutokana na kuchomwa visu mara 25 na mpenzi wake wa zamani.
Mbali na Profesa Mkenda, Jeshi la Polisi nalo limetoa taarifa kuhusu tukio hilo likimtaja Lucas Tarimo anayedaiwa kumshambulia Minja kwa kisu.
Ilivyokuwa
Ilielezwa katika mitandao ya jamii kuwa Beatrice na Tarimo waliwahi kuwa katika uhusiano wa kimapenzi, lakini uhusiano wao ulitawaliwa na migogoro hadi mwanamke huyo alipoamua kutengana na mtuhumiwa na kwenda kuanza maisha yake mapya.
Katika taarifa hiyo, ilielezwa kabla ya kuondoka mtuhumiwa anadaiwa kumpora Beatrice Sh10 milioni zilizokuwa za mtaji wa biashara pamoja na pesa za ujenzi wa nyumba ya mama yake na suala hilo liliripotiwa polisi, lakini mtuhumiwa inadaiwa hakukamatwa.
Pia ilidaiwa Beatrice alipoondoka aliacha baadhi ya mali, wakiwemo nguruwe wakubwa sita na vitoto 11 na baada ya kuondoka, Tarimo anadaiwa kwenda kwenye banda na kukatakata nguruwe wote pasipo kuchukuliwa hatua.
Ilidaiwa kuwa Novemba 13, 2023 saa 12 jioni, Beatrice akiwa na wanawake wengine wawili, walishambuliwa na mtuhumiwa ambaye alimkwida Beatrice na kumchoma jumla ya visu 25 maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Wasamaria wema walimwahisha Beatrice hospitali ya Huruma na kupatiwa rufaa kwenda KCMC ambako alilazwa hadi umauti ulipomkuta Desemba 26, 2023. Akiwa hapo alifanyiwa upasuaji mara mbili na kushonwa majeraha 20.
Taarifa zilizotolewa katika mtandao wa Facebook juzi zilisema shambulio hilo lilitokea Novemba 13, 2023, ikimtaja Paul Tarimo anayedaiwa kuwa mfanyakazi wa Waziri Adolf Mkenda.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime jana, ilisema tukio hilo liliripotiwa Polisi Novemba 12, 2023 na sio 13 na jina la mtuhumiwa ni Lucas Tarimo na sio Paul.
Katika taarifa hiyo, Misime alisema baada ya tukio hilo kuripotiwa Polisi, taratibu za ufuatiliaji zilianza kwa kupata maelezo ya wanawake wanaodaiwa kuwa pamoja na Beatrice siku ya tukio, sambamba na kumsaka mtuhumiwa ambaye alitoroka.
“Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa ambaye jina lake sahihi ni Lucas Tarimo. Shughuli zake ni fundi ujenzi wa nyumba anazofanya katika maeneo mbalimbali, ili aweze kukamatwa na hatua za kisheria kuchukuliwa,” alisema Misime.
Misime alisisitiza katika taarifa hiyo kuwa hakuna aliye juu ya sheria hata kama ana nafasi gani katika jamii au taifa na kutoa rai kwa mtu yeyote atakayemuona mtuhumiwa kutoa taarifa ili aweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Pia tunatoa tahadhari kwa yeyote anayemficha au anayemsaidia kuendelea kujificha akibainika hatua zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria,” alisema Misime.
Hata hivyo, jana taarifa zaidi zilizopatikana mitandaoni zilieleza kuwa, mtuhumiwa huyo kabla ya tukio hilo, aliwahi kumpiga Beatrice hadi akaharibu mimba na taarifa zilifikishwa Polisi Rombo, lakini mtuhumiwa hakukamatwa.
Jana Misime alipopigiwa simu na Mwananchi kuombwa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo, aliomba kutumiwa maswali kupitia WhatsApp na hata alipotumiwa, hakuyajibu, wala kupokea simu tena kila alipopigiwa.
Profesa Mkenda akanusha
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Moshi, Profesa Mkenda alisema:
"Nasikitika sana kwa jambo hili, na natoa pole kwa familia kwa msiba huu mkubwa sana na nitaenda kuwaona, najua kabisa polisi wamekuwa wakifuatilia jambo hili na mtuhumiwa anasakwa mchana na usiku.
“Tangu marehemu akiwa ni majeruhi nilikuwa nikiwasiliana na Jeshi la Polisi na najua kazi wanayoifanya ya kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa,” alisema.
Kuhusu jina la mtuhumiwa, Profesa Mkenda alikanusha kilichoandikwa mitandaoni, akisema mtuhumiwa sio Paul Tarimo, bali ni Lucas Tarimo kama ilivyoelezwa na polisi.
Pia alikanusha taarifa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa mfanyakazi wake, akisema: “Mtoa taarifa amezungumza kwamba mtuhumiwa ni mfanyakazi katika shamba langu, kwa kweli kijana huyu simfahamu kabisa na hajawahi kufanya kazi kwetu na Jeshi la Polisi limetuleza kwamba anafanya kazi ya useremala.
"Ninaomba raia wote wenye taarifa walishirikishe Jeshi la Polisi popote pale, kama unajua mtuhumiwa huyu ambaye Jeshi la Polisi limemtaja kama Lucas Tarimo popote alipo, toa taarifa polisi halafu watachukua hatua stahiki.”
Awali katika taarifa yake aliyoituma kwa njia ya sauti mitandaoni, Profesa Mkenda alionya tukio hilo kutumika kisiasa.
"Sisi wengine tujaribu sana kuondoa mambo ya kisiasa katika suala hili, kama una nia ya kumchafua mtu mpaka kufika mahali kutumia mauaji na kuuawa kwa ndugu yetu Beatrice kwa kweli ni kujishusha kwenye matope,” alisema.
Mtoto asimulia mwanzo mwisho
Alipotafutwa jana mtoto wa marehemu, Glory Mchomba alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea Novemba 12, mwaka huu mama yake huyo alikuwa anatokea kwenye kikundi na ndipo alipovamiwa na mwanaume huyo.
Alisimulia kuwa, ilikuwa Jumapili akiwa nyumbani, kuna mtu alimpigia simu akamwambia kuwa, mama yake yuko chini na hali yake sio nzuri na kumtaka kwenda kumpeleka hospitali.
“Nilishuka na mdogo wangu na kweli tukamkuta mama yuko chini na hali hali yake ilikuwa sio nzuri maana damu zilikuwa zikimtoka sana, tukaomba msaada wa pikipiki tukamshusha mpaka kituoni Tarakea (polisi) wakatuandikie PF3.
“Tukaenda naye mpaka hospitali ya Huruma tukaambiwa hawamuwezi, ikabidi wafanye taratibu za ambulance (gari maalum la kubeba wagonjwa), wakamleta KCMC tukawa tumefika usiku, ndio akafanyiwa matibabu.
"Wakati tuko njiani nilimuuliza mama nani kakufanyia hivyo akasema ni (anamtaja mtuhumiwa),” alisema.
Alisema walitoa taarifa polisi na walikuja hospitali na kumpiga picha na wakasema wapo kwenye upelelezi.
“Lakini mpaka sasa wako kimya hawajafanya uchunguzi wowote na hawajatupatia majibu na tukiwauliza wanasema kwamba hawajamwona na hawajui alipo bado wapo kwenye uchunguzi," alisema.
Aliongeza kuwa, wakati mama yake alipofikishwa KCMC, madakatari waliwaeleza kuwa mama yao amechomwa sehemu 25 mwilini mwake na kwamba baadaye hali yake ilibadilika na ndipo alipofariki Desemba 27, mwaka huu.