Matukio ya kujitoa uhai yalivyoacha maswali
Jeneza la kijana wa kimasai (morani) aliyedaiwa kujinyonga. Picha na Mohamed Hamad Kiteto
Dodoma. Wakati mwaka 2023 ukielekea ukingoni, Mkoa wa Dodoma bado una kumbukumbu ya mauaji ya kutisha ambayo yametokana na wivu wa mapenzi.
Matukio hayo ambayo yamegharimu maisha ya watu yametokea kwa nyakati tofauti na mengine kuzua taharuki kwa jamii kutokana na jinsi yalivyotendeka.
Miongoni mwa matukio yaliyovuta hisia ya watu wengi ni la wapenzi kukutwa wamekufa ndani huku miili yao ikiwa ina majeraha, na taarifa za polisi zikisema wapenzi hao waliuana kutokana na wivu wa mapenzi.
Hili linakuwa ni tukio la pili kutokea ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kwa wapenzi kuuawa katika Kata ya Dodoma Makulu jijini hapa.
Mengine ni mauaji ya kujinyonga ambayo kwa mwaka huu yameshika kasi baada ya watu wawili wakazi wa Mtaa wa Mahomanyika, akiwamo mtoto wa miaka 14 kujinyonga bila kuacha ujumbe wowote.
Matukio ya mauaji yapo mengi, hatuwezi kuyaorodhesha yote lakini kwa mwaka 2023 kulikuwa na matukio ya mauaji yaliyoripotiwa, ukiacha yale ambayo hayakuripotiwa kwenye Wilaya za Mpwapwa, Chamwino, Bahi, Chemba, Kondoa na Kongwa.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili juzi kuhusu mauaji yaliyotokea Kata ya Dodoma Makulu ya wapenzi wawili kukutwa chumbani wamekufa, Mwenyekiti wa Mtaa wa Msangalalee Magharibi, Lenard Ndama alisema matukio ya mauaji kwenye mtaa wake yamezua taharuki kubwa, hasa ya wapenzi kukutwa wameuawa ndani ya nyumba.
“Tumeliomba Jeshi la Polisi kuimarisha doria kwenye mtaa wetu maana kila tukio baya la mauaji linalotokea unasikia limetokea kwenye mtaa wetu, hadi polisi sasa wameshatujua wakisikia simu kutoka Makulu wanakuja mbio,” alisema Ndama.
Alisema wivu wa mapenzi ndiyo sababu kubwa ya mauaji mtaani kwake na kuwashauri vijana kama wameshindwa mambo ya mapenzi wafanye kitu kingine badala ya kung’ang’ania na mwisho wake yanasababisha mauaji.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mahomanyika, Ernest Kutona kulikotokea matukio ya watu watatu kujinyonga kwa kipindi cha mwezi mmoja, alisema hali hiyo imezua maswali mengi kwa jamii kutokana na wote waliojiua kutoacha ujumbe wa maandishi.
Alisema kwenye mtaa wake watu watatu, akiwamo mtoto mwenye umri wa miaka 14 walijinyonga bila kuacha ujumbe wowote wa maandishi uliosababisha kuchukua hatua ya kujitoa uhai.
Aliitaka jamii kukaa na ndugu zao wanaoonekana wana msongo wa mawazo ili waweze kujua kinachowasumbua kabla hawajafikia uamuzi wa kujitoa uhai
Mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Erasto Kano akizungumzia mauaji, alisema mengi yanasababishwa na msongo wa mawazo ambao husababisha mtu kujitenga na jamii, na hatimaye anafanya maamuzi magumu ya kujiua au kuua wenzake.
Dk Kano alisema matukio mengi ya mauaji hufanywa na watu ambao wamekosa ushauri kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki, hivyo kufanya uamuzi mgumu wa kujitoa uhai au kuwatoa wengine uhai wakidhani kuwa watapata nafuu ya maisha.
Aliishauri jamii kuwalea watoto kwenye misingi na mifumo mizuri ya malezi kwa kuwaacha wachangamane na watu wengine kwenye harusi, kanisani, misikitini na shuleni ili wanapokutana na matatizo waweze kuwaeleza watu wanaowazunguka kuliko kukaa kimya.
“Pia, kama mtu ana msongo wa mawazo na hawezi kumwambia mtu mwingine anatakiwa kwenda kanisani na kuongea na Mungu na kumweleza anayoyapitia kwa sababu inaaminika kwa kufanya hivyo unakuwa umeutua mzigo ulionao,” alisema Dk Kano.
Pia, alisema kitu kingine ambacho mtu mwenye hasira na msongo wa mawazo anaweza kukifanya ni kufanya mazoezi ya kukimbia, kusikiliza muziki, kuimba au kwenda kanisani na msikitini kupata uponyaji wa hisia.