Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Mkenda: Tuendeleze mazuri yaliyoachwa na waasisi wetu

Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda akishiriki futari na wananchi wa wilaya hiyo, hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Gosheni, wilayani Rombo.

Muktasari:

  • Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano wa kitaifa kwa kuenzi mazuri yaliyoachwa na waasisi wa taifa.

Rombo. Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ameeleza dhamira ya serikali kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuenzi misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa.

Profesa Mkenda ameyasema hayo wakati wa hafla ya futari aliyoiandaa kwa wananchi wa Wilaya ya Rombo, ikihusisha makundi mbalimbali ya dini na taasisi.

“Hii ndiyo sura halisi ya Tanzania, aliyoiacha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kila mmoja wetu ana imani yake, lakini tunashirikiana, kama ilivyo leo ambapo tumekutana kwa ajili ya futari. Hii ni ishara njema ya mshikamano wetu kama taifa. Nawashukuru wote mliohudhuria,” amesema Profesa Mkenda.

Akitilia mkazo umuhimu wa mshikamano, Profesa Mkenda amesema viongozi wa nchi wana jukumu la kuhakikisha jamii inaendelea kuwa na umoja bila ubaguzi wa aina yoyote.

“Ni ahadi yangu na ahadi yetu sote tuliopewa majukumu ya kulinda mshikamano huu. Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, amekuja na dhana ya 4R, inayosisitiza maridhiano na mazungumzo badala ya mifarakano. Tukikaa mezani na kujadiliana, hakuna jambo litakalotushinda,” ameongeza.

Kwa upande wake, Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaban Mlewa, amewasihi wananchi wa Rombo kuwaunga mkono viongozi wanaoshirikiana nao kwa karibu na kutatua changamoto zao.

“Naomba Wanarombo muiheshimu neema hii ya kuwa na Mbunge anayewajali. Wapo watu waliowachagua wabunge ambao hata hawajawahi kufika majimboni mwao, wala kupokea simu za wapiga kura wao. Tuendelee kushirikiana na viongozi wenye uchungu na wananchi,” amesema Shekhe Mlewa.

Aidha, aliwataka waumini kutumia mfungo wa Ramadhani kufanya mema na kuacha maovu ili kuboresha jamii.

“Nawaomba ndugu zangu tufunge kwa nia njema. Funga inaleta faida kiafya, lakini zaidi ya yote, inapaswa kutufanya waumini wa kweli. Tusiwe waumini wa msimu, ambao Ramadhani ikiisha, wanarudia maovu yao,” aliongeza Shekhe Mlewa.

Mchungaji Wilirk Herman wa Kanisa la The Sowers Evangelistic International Church (SEIC) Tarakea, amesisitiza pia mshikamano baina ya wananchi na viongozi, akisema amani ni nguzo ya maendeleo ya taifa.

“Tanzania ni yetu sote, lakini amani ni ya kwanza. Tupendane na tushikamane. Tunamshukuru Mbunge wetu kwa kutuandalia futari hii, ambayo ni ishara ya mshikamano na upendo kwa jamii yake,” amesema Mchungaji Herman.