Profesa Muhongo ataja maeneo sita yatakayobeba uchumi wa Tanzania
Muktasari:
- Takwimu za Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zinaonyesha uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.1 mwaka 2027 kutoka asilimia 5.4 mwaka huu, huku mfumuko wa bei ukiendelea kubaki katika viwango vya chini katika wigo wa Benki kuu ya Tanzania (BoT)
Dar es Salaam. Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo amependekeza Tanzania kuelekeza nguvu zake katika sekta sita za kimkakati ili kuharakisha ukuaji wa uchumi, kupunguza umasikini na kufikia lengo la kuwa uchumi wa dola trilioni moja katika miaka 25 ijayo.
Profesa Muhongo ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini amebainisha hayo leo Jumatatu, Juni 15, 2026 akiwa mchangiaji wa kwanza bungeni wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 ya Sh62.3 trilioni na taarifa ya hali ya uchumi.
Bajeti hiyo iliwasilishwa bungeni Juni 11, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- MIpango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo yeye akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi.
Katika mchango wake, Profesa Muhongo amesema pamoja na Tanzania kuendelea kufanya vizuri katika viashiria vya uchumi bado kasi ya ukuaji wa uchumi inahitaji kuongezeka ili kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wananchi.
Amesema takwimu za Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zinaonyesha uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.1 mwaka 2027 kutoka asilimia 5.4 mwaka huu, huku mfumuko wa bei ukiendelea kubaki katika viwango vya chini katika wigo wa Benki kuu ya Tanzania (BoT).
Hata hivyo, amesema wataalamu wa uchumi wanasema nchi zinazotaka kupunguza umasikini kwa kasi zinapaswa kuwa na ukuaji wa uchumi wa kati ya asilimia nane hadi 10 kwa mwaka.
“Kama tunataka kufuta umaskini kwa kiwango kikubwa lazima tuendeshe uchumi kwa maarifa na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi,” alisema.
Profesa Muhongo amesema eneo la kwanza linalopaswa kubeba uchumi wa Tanzania ni kilimo na viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao akipendekeza sekta hiyo ichangie angalau asilimia 30 ya Pato la Taifa.
Amesema pamoja na kilimo kuwa uti wa mgongo wa uchumi, bado nchi inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa mbegu bora na matumizi ya mbolea yapo chini.
“Mahitaji ya mbegu nchini ni tani 130,000 lakini bado kuna upungufu wa asilimia 50.8. Matumizi ya mbolea pia yapo chini ya kiwango kinachohitajika mtu anapaswa kutumia kilo 50 kwa hekta moja sasa mtu anatumia kilo 20, hivyo lazima tuwekeze zaidi katika pembejeo na kilimo cha umwagiliaji,” amesema.
Pia alitaka kuendelea kufanyika uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji ili kuhakikisha watu wanakuwa na uwezo wa kulima bila kutegemea msimu wa mvua.
Eneo lingine alilopendekeza ni gesi asilia ambalo amesema ni vyema kuhakikisha inachangia asilimia 25 ya Pato la Taifa kwa kuweka miundombinu itakayofanya gesi hiyo ilete matunda.
Alitolea mfano wa nchi ya Qatar ambayo kwa sasa asilimia 60 ya uchumi wake unatokana na gesi. “Tuna gesi nyingi lakini mchango wake katika uchumi bado ni mdogo. Qatar imejenga uchumi wake kwa kutegemea gesi na leo pato la mtu mmoja linafikia dola 73,000 kwa mwaka,” amesema.
Kwa upande wa madini, Profesa Muhongo alipendekeza sekta hiyo pamoja na viwanda vyake ichangie asilimia 20 ya uchumi, akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika madini ya kimkakati yanayohitajika katika teknolojia za kisasa.
Amesema dunia ya sasa inaelekea katika matumizi makubwa ya madini yanayohitajika katika utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki, teknolojia ya anga, sekta ya afya, usafirishaji na mageuzi ya nishati safi.
“Mbali na dhahabu, kuna madini mengi ya kimkakati ambayo dunia inayahitaji kwa sasa. Lazima tuyatambue na kuyaendeleza ili kuongeza thamani katika uchumi wetu,” amesema.
Muhongo alitaja utalii na viwanda vinavyohusiana na sekta hiyo kuwa eneo la nne huku akisema Tanzania inaweza kuongeza mapato ikiwa itawekeza katika huduma na miundombinu.
Alitolea mfano wa Morocco na Misri ambazo zimefanikiwa kuvutia zaidi ya watalii milioni 19 kila mwaka na kuingiza zaidi ya dola 11 bilioni za Marekani na dola 15 bilioni za Marekani mtawalia.
Katika uvuvi na ufugaji pamoja na viwanda vyake amesema vinaweza kuchangia asilimia tano ya uchumi iwapo vitaendelezwa kisasa zaidi.
Amesema upo umuhimu wa kuwekeza katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, usindikaji wa samaki na bidhaa za mifugo ili kuongeza thamani na mapato ya mauzo ya nje.
Sekta ya sita aliyotaja ni rasilimali watu, akisema Watanzania wanapaswa kupewa elimu bora na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la kimataifa ili waweze kuongeza mapato ya fedha za kigeni kupitia ajira nje ya nchi na kuchangia asilimia tatu ya Pato la Taifa.
Ametolea mfano wa fedha zinazotumwa na watu wanaofanya kazi nje ya mataifa yao, ambapo amesema takwimu zinaonyesha kuwa India iliingiza dola bilioni 135 za Marekani mwaka jana, huku Kenya ikiingiza zaidi ya dola 5 bilioni za Marekani.
“Lazima tuwasomeshe watoto wetu vizuri ili waweze kushindana duniani na kuingiza fedha kutoka nje ya nchi,” amesema.
Katika sanaa na michezo amelitaja kuwa eneo lingine la kimkakati kutokana na uwezo wake wa kuzalisha ajira, mapato na kuvutia uwekezaji huku akitaka ichangie asilimia mbili.
Mbali na yote Profesa Muhongo amesema mafanikio ya sekta hizo yatategemea uwepo wa umeme wa uhakika, wa kutosha na wa gharama nafuu pamoja na kuimarisha akiba ya dhahabu ya taifa ili kuongeza uthabiti wa uchumi.
“Bila umeme wa uhakika na akiba ya kutosha ya dhahabu, itakuwa vigumu kufikia uchumi mkubwa na shindani tunaoutamani,” amesema.