Raia 59 wa Burundi jela, washindwa kulipa faini

Muktasari:

  • Raia 59 wa Burundi wamelazimika kuanza kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kushindwa kulipa Sh500, 000 kama faini baada ya kukutwa na hatia ya kuingia na kuishi nchini kinyume na sheria.

Dar es Salaam. Raia 59 wa Burundi wamelazimika kuanza kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh500, 000; iliyokuwa imeamriwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mahakama hiyo iliwahukumu raia hao kulipa faini hiyo au kwenda jela mwaka mmoja baada ya wao kukiri makosa ya kuingia na kuishi nchini kinyume na sheria.

Pia mahakama hiyo imetoa amri kuwa baada ya raia hao kutumikia adhabu hiyo, warudishwe nchini kwao.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi, Ushindi Swalo, ambaye amesema: “Washtakiwa wamekiri mashtaka ya kuingia nchini bila kibali maalumu, na kuishi kinyume na sheria...baada ya washitakiwa kukiri makosa yanayowakabili, mahakama inawahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh500, 000.”

"Ili iwe fundisho kwa wengine Kwa sababu haya makosa yamekithiri, hivyo mnatakiwa kulipa faini ya Sh500, 000 au kwenda jela miezi 12 na pia baada ya kutumikia adhabu hiyo warudishwe nchini kwao," amesema Hakimu Swalo.

Awali Wakili Mkuu Mwandamizi wa Serikali, Godfrey Ngwijo, aliwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao ambapo walikiri makosa yanayowakabili.

"Naiomba mahakama hii itoe adhabu kali kulingana na sheria ili iwe fundisho kwa wengine," alidai Ngwijo.

Hata hivyo washitakiwa hao wameshindwa kulipa faini hiyo na wamepelekwa gerezani kutumikia kifungo hicho kama ilivyoamuriwa na mahakama.

Katika kesi ya msingi, inadaiwa kuwa Juni 13,2023 eneo la Jangwani, jijini Dar es Salaam, washitakiwa  walikutwa wameingia na kuishi nchini bila ya kibali kutoka ofisi ya uhamiaji.