Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Raia wa China akamatwa kwa kuwashambulia wafanyakazi Morogoro

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo.

Muktasari:

  • Raia wa China anayefanya kazi katika Kampuni ya TBEA amekamatwa kwa tuhuma za kuwashambulia kwa kutumia kitu butu wafanyakazi wenzake wawili katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia raia wa China anayefanya kazi katika Kampuni ya TBEA, kwa tuhuma za kuwashambulia wafanyakazi wenzake wawili katika Wilaya ya Mvomero, huku likiendelea kumtafuta mshukiwa mwingine anayedaiwa kushiriki katika tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 20, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Endrew Kantimbo amesema mtuhumiwa anayeshikliwa ni Zhou Zhi (36), fundi minara katika Kampuni ya TBEA.

Amesema tukio hilo lilitokea Juni 19, 2026 katika Kitongoji cha Sokoine Ranch, Kijiji cha Wami Sokoine, Kata ya Dakawa, Wilaya ya Mvomero, ambapo Zhou Zhi akishirikiana na raia mwenzake wa China anayefahamika kwa jina la Yung Lu, waliwashambulia wafanyakazi hao kwa kutumia kitu butu.

Waliojeruhiwa ni Stephen Mwampaka (44), dereva wa Kampuni ya TBEA, pamoja na Mbaraka Ally (18), ambaye ni kibarua katika kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Kantimbo, waathirika hao walipata majeraha katika sehemu mbalimbali za miili yao na walipatiwa matibabu na chanzo cha tukio hilo kinaendelea kuchunguzwa na Jeshi la Polisi.

Amesema mtuhumiwa Zhou Zhi anaendelea kushikiliwa katika Kituo cha Polisi Mvomero kwa ajili ya mahojiano na hatua nyingine za kisheria, huku juhudi za kumkamata Yung Lu zikiendelea.

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi linawashikilia Fadhili Nyambalo (19) pamoja na watuhumiwa wengine kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa pikipiki tatu aina ya Haojue na uporaji wa simu za mkononi, yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mvomero kati ya Mei 21 na Mei 28, 2026.

Kamanda Kantimbo amesema matukio hayo yalitokea katika Kitongoji cha Kingurungunda, Kijiji cha Mbigiri na Kitongoji cha Sokoine Ranch, Kijiji cha Wami Sokoine, Kata ya Dakawa, ambapo watuhumiwa wanadaiwa kutekeleza vitendo vya uporaji na wizi.

Amesema uchunguzi wa matukio yote unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.