Rais aagiza Uhamiaji kudhibiti urasimu kwa wageni

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na aiongozi na askari wahitimu wa Mafunzo ya Awali Kozi Na. 1/2022 ya Jeshi la Uhamiaji pamoja na wananchi katika Hafla ya ufungaji wa mafunzo hayo iliyofanyika katika Chuo cha Uhamiaji.

Muktasari:

  • Rais Samia amemwagiza Kamishna wa Uhamiaji nchini kudhibiti urasimu katika utoaji wa vibali vya kuishi kwa wageni wachukuliwe hatua kali.

Mkinga. Rais Samia Suluhu Hassan amemwagiza Kamishna wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala kudhibiti urasimu katika utoaji wa vibali vya kuishi nchini kwa wageni ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa kigeni kufanya shughuli zao bila bugdha.

Maelekezo hayo aliyatoa leo Agosti 15 wakati akifunga mafunzo ya kwanza Kwa askari wa uhamiaji 818 katika chuo cha Bomakichaka kilichopo wilayani Mkinga mkoani Tanga.

Amesema sasa nchi imefunguka hivyo kutakuwa na ujio wa wageni wengi kutoka nchi mbalimbali ambazo wanakuja nchini Kwa ajili ya kuangalia fursa  mbalimbali za uwekezaji ikiwemo utalii.

Hivyo amesema usumbufu wa upatikanaji wa vibali hivyo unasababisha vikwazo kwa wageni hao na hivyo kurudisha nyuma juhudi za serikali ya kuweka mazingira mazuri Kwa wageni kuja nchini.

"Punguzeni urasimu katika utoaji wa visa kwani Kwa Sasa inapatikana kupitia njia ya mtandao hivyo hakuna haja Wala sababu za uchekeweshaji ambao unasababisha usumbufu Kwa wageni," amesema Rais Samia.

Aidha, Rais amemwagiza Kamishna wa uhamiaji kuwa chukulia hatua Kali za kinidhamu maofisa watakaobainika kusababisha upotevu wa mapato katika taasisi hiyo.

"Huko kwenye vituo vya kazi kuna kiasi kikubwa cha maofisa wengi kuhusika na vitendo vya kupokea rushwa, vitendo vya unyanyasaji kwa wageni na wananchi hivyo vishughulikieni Ili kuweka taswira nzuri ya jeshi," amesema Rais Samia.

Vile vile katika kuongeza ufanisi katika utendajikazi akimtaka Kamishna kuwachanga watumishi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara badala ya kubaki kwenye vituo vyao Ili kuongeza tija katika ufanyajikazi wao.

Awali Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema kuwa Rais alifanya mabadiliko katika Jeshi la Uhamiaji kutokana na ongezeko la bajeti waliyopewa kwa lengo la kuongeza ufanisi.

Pia amebainisha kuwa walitengewa Sh600 bilioni kwa ajili yakujenga nyumba za watumishi na kuboresha miundombuni ya chuo hicho.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala amesema kuwa wanatarajia kuanzisha mafunzo Maalum ya ulinzi wa bahari ili kukabiliana na wahamiaji haramu.

Kutokana na mkakati huo, amesema wameomba kibali cha kuongezewa ekari 284 kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo katika chuo hicho.

Aidha Kamishna Makakala amebainisha kuwa katika kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa uhamiaji hapa Nchini idara ya uhamiaji wanatarajia kujenga chuo kipya cha mafunzo ya uongozi Kwa ajili ya watumishi wake.

"Kutokana na maboresho makubwa likiwemo ongezeko la bajeti, kumesaidia kuongeza ari ya utendajikazi Kwa watumishi na hivyo kuwezeshwa kuongeza makusanyo ya mapato hadi kufikia Sh189.5 bilioni katika mwaka wa fedha uliopita," amesema Dk Makakala.

Naye Mkuu wa mkoa wa Tanga Omar Mgumba amesema tayari wameanza kuifanyia kazi changamoto ya mawakala wa wahamiaji haramu ambao wamekuwa wanatumika kusafirisha watu hao.

Amesema uchunguzi wao wameweza kubaini baadhi ya watumishi wa serikali kutumika katika biashara hiyo haramu Kwa kutumia vyombo vya umma katika utekelezaji wa jambo hilo.

"Tayari tumekamata.mawakala ambao ni watumishi wa umma ambao wanajihusisha katika kusafirisha wahamiaji haramu katika mkoa wetu na tutawachukulia hatua Kali za kisheria Ili kuwaelewesha uadilifu katika utumishi wa umma," amebainisha RC Mgumba.

Aidha Mkuu wa mkoa huyo ametaja changamoto ya mrudikano wa wahamiaji haramu ambao wamemaliza vifungo vyao imekuwa ni kikwanzo kutokana na kutumia raslimali za nchi yetu.