Rais Samia aagiza maofisa uhamiaji wenye vitambi kurudi vyuoni

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na aiongozi na askari wahitimu wa Mafunzo ya Awali Kozi Na. 1/2022 ya Jeshi la Uhamiaji pamoja na wananchi katika Hafla ya ufungaji wa mafunzo hayo iliyofanyika katika Chuo cha Uhamiaji.

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amesema maofisa wa jeshi hawatakiwi kuwa na vitambi, hivyo amelitaka Jeshi la Uhamiaji kuweka utaratibu kwa maofisa hao kurudi vyuoni ili kupata mafunzo yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza maofisa wa Jeshi la Uhamiaji waliopo kwenye vituo mbalimbali nchini, kurudi vyuoni kwa ajili ya kupatiwa kozi fupi za kuwajengea uwezo katika kazi zao.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo Agosti 15, 2022 katika wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wakati akizindua chuo cha mafunzo cha Jeshi la Uhamiaji cha Boma Kichakamiba ambacho kilianzishwa mwaka 2020.

Amesema Serikali yame imetoa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo kwa maofisa kwa sababu wameona maofisa wa Tanzania wa vikosi vyote, kwa muda mrefu hawajapitia mafunzo hayo.

“Kwa hiyo tumetoa fedha nyingi ili maofisa warudi vyuoni, waje kupata tena mafunzo. Wapate refresher courses (kozi fupi). Wamesoma kozi za awali, wamemwagwa vituoni, wanafanya kazi zao lakini wanafanya kwa uzoefu. Kwa hiyo warudi hapa au vyuo vya majeshi mengine.

“Warudi wapate refresher courses, wapigwe msasa. Warudi tena kwenye vituo vyao ili wale wapya wakiingia wako vizuri, wale walioko vituoni wapigwe msasa ili wakiungana wote wanakuwa vizuri, jeshi linakuwa linafanya kazi vizuri,” amesisitiza Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi, amebainisha kwamba baadhi ya maofisa wa jeshi wana vitambi, hivyo anaona hiyo ndiyo fursa kwa maofisa hao kuondoa vitambi vyao kwa sababu hawatakiwi kuwa na vitambi.

“Kwa hiyo hiki chuo kisipoe, kwa mazingira yoyote yaliyopo. Nilikuwa naangalia gwaride, waliokuwa wakiongoza vikosi vile ni maofisa ambao ni wazoefu, kati yao kuna wenye vitambi, nimeviona vitambi hapa.

“Nadhani hatutakiwi kuwa na maofisa wa vitambi, warudi tena hapa, waje watoe vitambi ili wawe wepesi zaidi katika kutimiza kazi zao,” amesisitiza Rais Samia ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema mapinduzi ya kibajeti ni makubwa na katika Jeshi la Uhamiaji kuna ongezeko la asilimia 42, kutoka Sh66 bilioni hadi Sh93 bilioni ambapo ndani yake kuna fedha za mafunzo.

“Katika uongozi wako umeweka historia kubwa. Umekubali marekebisho ya sheria kuifanya idara yetu ya uhamiaji kuwa jeshi kamili. Lakini umeweka historia, Jeshi la Uhamiaji linafanya mafunzo katika chuo chake chenyewe,” amesema Masauni.

Waziri huyo amesisitiza kwamba mabadiliko hayo tafsiri yake ni kwamba sasa Jeshi la Uhamiaji linakwenda kwenye stahiki na marupurupu yanayofanana na majeshi mengine, jambo ambalo litawaongezea ufanisi zaidi.