Rais atia neno ukata mifuko ya wafanyakazi

Thursday April 08 2021
ukatapic
By Peter Elias

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) una hali mbaya, hivyo Serikali ina kazi ya kufanya kuunusuru.

Rais Samia alisema hayo jana Ikulu Dar es Salaam, katika hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu wao aliowateua Aprili 4, huku akiwapa maelekezo sambamba na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma.

Kauli hiyo ya Rais Samia imekuja wakati kukiwa na malalamiko kwa wastaafu katika sekta ya umma kutolipwa mafao yao kwa wakati na kusababisha wengi kuishi kwa shida.

Akitoa maelekezo kwa Masha Mshomba ambaye ni mkurugenzi mkuu mpya wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Rais Samia alisema kutokana na hali mbaya ya mfuko huo, hakufanya uteuzi wa kiongozi wake mpaka pale mambo yatakapowekwa sawa.

“Najua hali ya PSSSF, mfuko una hali mbaya sana, najua, na ndiyo maana sikuteua mtu,” alisema Rais Samia.

“Tuna kazi ya kufanya kwanza kuhusu mfuko ule, halafu sasa ndiyo tutapanga safu ya kushika mfuko huo.”

Advertisement

Kuhusu mfuko wa NSSF, Rais Samia alimwelekeza Mshomba kwenda kuusimamia vizuri mfuko huo ili sekta binafsi irudishe imani na wawaingize wafanyakazi wao katika mfuko huo ambao ni maalumu kwa ajili yao.

“NSSF ni mfuko wa `private sector’ (sekta binafsi). Private sekta ndiyo injini ya uchumi wa nchi, hapa makelele yote ninayopiga ni kuvuta private sector na huo ndio mfuko wao, naomba ukausimamie vizuri.

“Na uhakikishe `private sector’ inawaingiza Watanzania wote wanaowaajiri. Asitoke Mtanzania hana pesa yake mwisho wa huduma yake kwenye shirika au kampuni,” alisema Rais Samia akitoa agizo kwa mkurugenzi huyo wa NSSF.

Rais Samia alisema hayo wakati kukiwa na malalamiko ya wastaafu katika utumishi wa umma kutolipwa kwa wakati mafao yao baada ya kustaafu. Wastaafu hao wamekuwa wakilalamika kutolipwa mafao yao kwa zaidi ya miezi sita tangu wastaafu. Februari 26, Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli alichukizwa na kitendo cha wastaafu wa Jeshi la Polisi kucheleweshewa mafao yao licha kuwa fedha zao zipo, huku akiibebesha lawama Wizara ya Mambo ya Ndani na kuitaka ishughulikie suala hilo haraka.

Hata hivyo, hicho kimekuwa kilio cha muda mrefu kwa watumishi wengi wa umma wanaostaafu na kutolipwa mafao yao kwa wakati ili yawawezeshe kuendesha maisha yao ya uzeeni.

Akizungumzia suala hilo, mwalimu wa sekondari ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema wamekuwa wakisikia malalamiko ya wenzao wanaostaafu kucheleweshewa mafao yao, jambo linalosababisha maisha yao kuwa magumu.

“Namuomba Rais Samia afanyie kazi huo mfuko wetu, kuna tatizo. Kustaafu si jambo la dharura, kwa nini mafao yanachelewa wakati inajulikana mwaka fulani wanaostaafu ni watu kadhaa,” alisema mwalimu huyo.

Advertisement