Rais Museveni aruhusu NMG kurejea Uganda, Rostam asema…
Muktasari:
- Hatua hiyo inakuja mwezi mmoja tangu mamlaka nchini humo, zitangaze kusitishwa kwa huduma za vyombo vya habari vya kampuni hiyo, ambavyo ni Daily Monitor na NTV. Taarifa hiyo ilitolewa na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Dar es Salaam.
Hatua hiyo inakuja mwezi mmoja tangu mamlaka nchini humo, zitangaze kusitishwa kwa huduma za vyombo vya habari vya kampuni hiyo, ambavyo ni Daily Monitor na NTV. Taarifa hiyo ilitolewa na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Katika taarifa yake ya kusitisha huduma ya vyombo hivyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Muhoozi aliandika, “Daily Monitor na NTV Uganda hazitafunguliwa tena bila ruhusa yangu.”
Aliongeza:“Nchini Uganda, siamini katika uhuru wa vyombo vya habari! Vyombo vya habari vinapaswa kuongozwa na makada wa Mapinduzi.”
Pia aliongeza:“Kufungwa kwa NTV na Monitor ni mwanzo tu. Tutawakamata watu wengine wengi zaidi.”
Katika taarifa yake kwa umma leo, Jumanne Julai 28, 2026 Kampuni ya Taifa Group inayomiliki Nation Media Group (NMG), imeeleza hatua hiyo ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano wa kikanda, hasa kwenye uwekezaji, biashara na ukuaji wa tasnia ya habari Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Taifa Group, Rostam Aziz, amemshukuru Rais Museveni kwa uamuzi huo, akisema umeonyesha umuhimu wa mazungumzo, kuheshimiana na diplomasia katika kutatua changamoto katika uwekezaji wa kikanda.
Rostam, ametoa pongezi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (UPDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kwa mchango wake katika mchakato wa mazungumzo yaliyofanikisha kufikiwa kwa makubaliano hayo.
“Uamuzi huu unaonyesha nguvu ya mashauriano na ushirikiano katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji na maendeleo ndani ya Afrika Mashariki,” amesema Rostam.
Amesema Taifa Group inaendelea kuunga mkono misingi ya uandishi wa habari unaozingatia weledi, uhuru, uwajibikaji na usawa, akibainisha kuwa vyombo vya habari vina nafasi katika kukuza uwazi, utawala bora na maendeleo ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NMG, Joe Muganda, amesema kurejea kwa huduma za kampuni hiyo Uganda ni mwanzo mpya wa kujenga uhusiano na wasomaji, watazamaji, wasikilizaji pamoja na washirika wa kibiashara.
Amesema hatua za awali zitahusisha kurejesha mifumo ya uchapishaji, utangazaji na uzalishaji wa maudhui kupitia magazeti, redio, televisheni na majukwaa ya kidijitali.
Amesisitiza NMG itaendelea kuwekeza katika maudhui ya ndani yanayoaminika na yanayolenga kuleta mijadala yenye tija kwa jamii.
“Tunatazamia kushirikiana tena kwa karibu na wadau wetu nchini Uganda ili kuendeleza safari ya kutoa taarifa zenye ubora na zinazojenga jamii,” amesema Muganda.
Kurejea kwa NMG nchini Uganda kunakuja wakati nchi za Afrika Mashariki zikihimiza zaidi uwekezaji unaovuka mipaka kama sehemu ya kukuza biashara na ushirikiano wa kiuchumi.
NMG, yenye mtandao katika nchi za Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda, imekuwa miongoni mwa vyombo vya habari vikubwa Afrika Mashariki kwa miongo kadhaa, ikihudumia jamii kupitia magazeti, televisheni, redio na majukwaa ya mtandaoni.
Kwa upande wake, Taifa Group ni kampuni ya uwekezaji inayojihusisha na sekta mbalimbali zikiwemo mawasiliano, nishati, madini, miundombinu, usafiri wa anga, kilimo na vyombo vya habari.
Taarifa hiyo, imesisitiza Taifa Group itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuwezesha uwekezaji, ajira na ukuaji wa uchumi endelevu ndani ya Afrika Mashariki.