Rais Mwinyi ainadi Z’bar China, ataja fursa ikiwemo bandari

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Han Zheng leo Juni 20, 2023
Unguja. Rais wa Dk Hussein Mwinyi akunata na kufanya mazungumzo na Han Zheng Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, huku akinadi fursa zilizopo visiwani humo.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamefanyika leo Juni 28 2023, viongozi hao wamepongeza ushirikiano unaoendelea kati ya Tanzania na China na Zanzibar kwa upande mwingine.
Rais Mwinyi ameipongeza Serikali ya hiyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi ya maendeleo kwa miaka 59 sasa tangu Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Dk Mwinyi amebainisha uamuzi wa hivi karibuni wa viongozi wakuu wa nchi hizi mbili Samia Suluhu Hassan na Xi Jing Ping wa kufungua zaidi njia kuu za uhusiano ambazo zimesaidia kuimarisha uhusiano huo.
Aidha Rais Mwinyi amemweleza Makamu huyo wa Rais wa China sera kuu ya Zanzibar ya uchumi na kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchi hiyo kusaidia katika uwekezaji.
"Kuna sekta ya utalii, mradi wa ujenzi wa bandari kubwa ikiwemo ya Mangapwani itakayonufaisha mataifa mengine ya Afrika, uchimbaji wa mafuta na gesi, uvuvi na usafiri wa baharini," amesema.
Kwa upande wa makamu huyo, alimhakikishia Dk Mwinyi kwamba nchi yake imejizatiti kuiunga mkono Zanzibar kufikia hatua kubwa ya maendeleo ambapo amesema kwa sasa Serikali yao inawahimiza watalii wengi wa China kuitembelea Zanzibar.
Zhang amempongeza Rais Dk Mwinyi kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya maendeleo na kusema chini ya uongozi wake Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo.
Kesho Alhamisi Juni 29, 2023 Rais Mwinyi akiendelea na ziara ya nchini China anatazamiwa kuhudhuria maonesho makubwa ya tatu ya China na Afrika yaitwayo China- Africa Economic and Trade Expo katika jijini Changsha na baadaye atakuwa na mkutano maalumu katika sekta ya afya.