Rais Samia aeleza siri ya Uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar

Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Uhuru wa Tanganyika ulikuwa chachu na mchango muhimu katika kuwezesha mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Uhuru wa Tanganyika ulikuwa chachu na mchango muhimu katika kuwezesha mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Amesema matukio hayo mawili yaliyotangulia Muungano ndiyo yaliweka msingi imara wa nchi na Taifa imara la sasa, lenye amani, mshikamano na umoja miongoni mwa watu wake.

“Tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kutujaalia uzima wa kuiona siku hii ya kihstoria katika Taifa leo,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatano Desemba 8, 2021 wakati akilihutubia Taifa ikiwa ni saa chache kabla ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika uliopatikana Desemba 9, 2021.

#LIVE: RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKILIHUTUBIA TAIFA

Rais Samia amesema kwa takwimu za watu, Watanzania takribani milioni 2.52 kati ya hao milioni 59 waliopo leo sawa na asilimia 4.3 ya watu wote ndiyo walikuwa wamezaliwa kabla ya Desemba 9, 1961.

Hiyo ikiwa ina maana kuwa sehemu kubwa ya Watanzania wanaoadhimisha miaka 60 ya Uhuru ifikapo Desemba 9, 2021, wanaweza wasipate tena fursa ya kuadhimisha makumi mengine yajayo ya maadhimisho haya.

“Tunaoshuhudia siku hii ya leo, tujione ni kati ya wenye bahati. Takwimu hizi zinatuambia jambo lingine muhimu kuwa Watanzania wengi waliopo leo si tu hawakuwepo wakati wa Uhuru bali tu hawakuyaishi madhila ya ukoloni na matokeo yake,” amesema.

Siri ya mafanikio

Katika hotuba hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka 60 ya Uhuru yamebebwa na utawala wa demokrasia na sheria.

Amesema wakati wa uhuru kulikuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa ambao, baadaye mwaka 1962 ulifutwa ili kujenga umoja na mshikamano wa nchi kwanza.

Baadaye mfumo huo ulirejeshwa tena mwaka 1992 baada ya nchi kupiga hatua kubwa katika utawala wa sheria na maendeleo ya kiuchumi.

“Tangu kurejea mfumo wa vyama vingi, vipo vyama 16 vilivyosajiliwa na 17 vinavyoomba usajili wa muda. Tumekuwa na mfumo bora unaoheshimiwa na imara wa kuweka viongozi madarakani kupitia chaguzi za kila baada ya miaka mitano,” amesema.

Pia amesema kuwa wananchi wamekuwa na haki ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka na kuchaguliwa pindi wanapotaka kushika madaraka katika ngazi tofauti za uongozi.

“Wakati wa uhuru nchi ilikuwa na wabunge 80 ukilinganisha na nafasi za wabunge 393 na waliopo ni 391, kati ya hao wanawake ni wabunge 143 na wanaume ni 248.

“Kama nchi imeendelea kulinda na kuheshimu na kulinda haki za msingi za binadamu na watu kwa kuweka mifumo ya kuwezesha wananchi kutoa maoni kwa uhuru bila kubugudhiwa,” ameongeza Rais Samia ambaye ameweka historia ya kuwa Rais wa Kwanza mwanamke katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, Rais Samia amesema vimeendelea kuwa huru na hadi sasa magazeti na majarida yaliyosajiliwa nchini yamefikia 270, redio 198, redio za mtandaoni zaidi ya 200, blog 120, televisheni 51, televisheni za mtandao zaidi ya 500 ikilinganishwa na chombo kimoja wakati wa uhuru.

Safari ya Tanganyika hadi uhuru

Rais Samia amesema Tanganyika imekuwa na safari ndefu ndefu baada ya uhuru ikiwamo kutoka katika kundi la nchi maskini hadi kufikia uchumi wa kati wa chini.

Amesema safari ya kutoka uchumi wa kati wa chini kwenda uchumi wa katikati na badaye uchumi wa juu si ndefu sana huku akisema kazi inayofanyika itakuwa ni chachu ya kufika huko

“Wito wangu kwenu ni kuendelea kudumisha amani, umoja, mshikamano na Muungano wetu, kuendelea kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu na kufanya mageuzi ya kiuchumi kila inapolazimu kuendana na kasi ya uchumi wa dunia,” amesema Samia.

Amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira na kuyalinda kwa wivu mkubwa ili kurithisha vizazi vijavyo nchi yenye neema kama ilivyopokelewa kwa vizazi vilivyotangulia.

Amesema dira ya maendeleo ya mwaka 2025 inaelekea kumalizika huku uchumi wa nchi unatarajiwa kukua kwa asilimia 8.

“Tunapoangalia mbele, tunakwenda kuandaa dira ya miaka 25 ijayo ambayo itatutoa mwaka 2025 hadi mwaka 2050, itaelekeza kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kwa kutoa kipaumbele sekta zinazogusa wananchi moja kwa moja,” amesema.