Rais Samia aguswa na uwajibikaji wa NBC kwa jamii

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuguswa na hatua ya taadisi za fedha katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.







Mwandishi Wetu



Zanzibar. Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuguswa na hatua ya taasisi za fedha nchini katika kujenga mfumo jumuishi wa fedha na uwezeshaji makundi mbalimbali ya wananchi kiuchumi.

Samia ameyasema hayo leo Septemba 4, 2022 alipozindua jengo la ofisi ya Saccos ya Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja, visiwani Zanzibar ambapo pia alipokea samani mbalimbali zilizotolewa na Benki ya NBC kwa ajili ya saccos hiyo.

Ameipongeza NBC na benki nyingine kwa kuchochea uchumi jumuishi huku zikitumia sehemu ya mapato yao kurejesha kwa jamii kupitia misaada inayoitoa.

“Naamini kupitia Saccoss hii ya Kizimkazi wananchi wengi wa eneo hili watafikiwa na huduma muhimu za kifedha na hivyo kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa kaya nyingi za eneo hili. Nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Benki ya NBC kwa namna ilivyoguswa na jitihada za wakazi hawa wa Kizimkazi na hivyo kuamua kuwaunga mkono kwa kuwapatia msaada wa samani za ndani ikiwemo viti na meza kwa ajili ya ofisi yao...hongereni sana benki ya NBC,’’ amesema Samia.

Amewata wananchi kutumia vema ushirikiano na taadisi hizo za fedha, ili kujikwamua kupitia misaada hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi amesema msaada huo ni mwendelezo wa jitihada za benki hiyo katika kuiunga mkono serikali.

“Kupitia Saccoss hii wananchi wanakwenda kufikiwa na huduma za kifedha, hatua ambayo itawawezesha kupata mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji yao ya kibiashara na kujiongezea kipato kwa faida ya uchumi wao na familia zao," amesema.

Amesema si mara ya kwanza kwa benki hiyo kushirikiana na wakazi wa Kizimkazi katika miradi ya maendeleo, kwani iliwahi kushiriki ujenzi wa madarasa ya shule ya awali Kizimkazi-Mkunguni na utoaji msaada wa gari maalum la tiba kwa ajili ya huduma bure kwa mama na mtoto visiwani humo.


“Misaada yote imekuwa na matokeo chanya kwa jamii hii na sisi kama Benki na mdau wa maendeleo, tunajivunia sana kuwa sehemu ya suluhu ya changamoto za jamii yetu," amesema.

Akitoa taarifa kuhusu Saccos hiyo, Mratibu wa Saccos ya Kimzikazi, Said Ramadhani Mgeni amesema kukamilika kwa mradi huo uliokwama mwaka 2015, kunatka fursa kwa wakazi wa eneo Hilo kuhifadhi fedha eneo karibu na makazi yao.

“Kukamilika kwa mradi huu kunatoa fursa kwa wananchama na wakazi wa vijiji jirani kuihifadhi fedha karibu kabisa na makazi yao huku pia ujenzi wa ofisi hiyo ukitarajiwa kutoa huduma ya ukumbi kwa wakazi kizimkazi.

"Tutakapokuwa na mikutano yetu na kwenye hili tunawashukuru sana Benki ya NBC kwa msaada wao wa samani za ndani ikiwemo viti na meza ambavyo tunaahidi kuvitunza na kuvilinda’,’ amesema.