Rais Samia aidhinisha Sh15.4 bilioni fidia Liganga, Mchuchuma
Muktasari:
- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aidhinisha fedha za malipo ya fidia kwa Wananchi wa Mchuchuma na Liganga, Wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe.
Ludewa. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, aidhinisha fedha za malipo ya fidia kwa Wananchi wa Mchuchuma na Liganga, Wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe.
Hayo yamebainishwa na Afisa Mwandamizi kitengo cha Mipango Shirika la Maendeleo la Taifa Florian Mlamba, alipo kuwa akizungumza na wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara uliofanyka Kata ya Mundindi.
Amesema kiasi cha Sh15.4 bilioni kimeidhinishwa kwaajili ya malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha maeneo yao kwaajili ya miradi ya Mchuchuma na Liganga.
Pia amewaomba wananchi hao kutoa ushirikiano wa kutosha ili kukamilisha zoezi mapema na kuingiziwa fedha zao.
“Tunaomba ushirikiano wenu, na kwa kadri tutakavyo maliza mapema, ndivyo na fedha za malipo zitaingizwa kwenye akaunti zenu mapema na matarjio yetu mwezi huu mwishoni tuwe tumeishaziingiza.” Amesema Mlamba.
Ameongeza kuwa fedha zote zitalipwa kwa njia ya benki hivyo kila mnufaika wa fidia hizo lazima awe na akaunti ya benki kwa ajili ya malipo hayo.
Kwa upande wake Mbunge wa Ludewa Joseph Kamonga amewataka wananchi hao kutumia fedha hizo kwaajili ya uwekezaji.
“Fedha hizo zikiingia , zitumieni vizuri; zisiwachanganye , fanyeni uwekezaji lakini pia mnavyohama, basi zingatieni na athari za kimazingira,” amesema Kamonga
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ludewa, Grevas Ndaki, amewataka wananchi kulinda mila na desturi zao.
“Zingatieni mila na desturi zenu, msikengeuke na mila za wageni watakao kuja na miradi ya uwekezaji utakao fanywa katika mazingira yenu.”
“Lakini pia jikingeni na maradhi kutokana na ongezeko la watu litakalokuja hapa kufuatia uwekezaji unaotarajiwa kuja,” ametahadharisha Ndaki.