Rais Samia aigusa Tanesco, atengua wengine watatu

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko kwa baadhi ya viongozi huku akiigusa nafasi mbali mbali ikiwemo Tanesco pamoja na wakuu wa wilaya.

Dar es Salaam. Wakati changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini ikiendelea kushika kasi, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya viongozi wa Shirika la Umeme (Tanesco) pamoja na utenguzi na uteuzi wa viongozi mbalimbali alioutangaza leo Septemba 24, 2023.

Taarifa kwa umma iliyotolewa inaeleza kuwa Rais Samia amemteua Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco huku aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo Omar Issa ikielezwa kuwa ataendelea na majukumu mengine aliyopangiwa katika Ofisi ya Rais - Tume ya Mipango.

Rais Samia amemteua Gissima Nyamo-Hanga kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Kabla ya uteuzi huo Nyamo - Hanga aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).

Maharage Chande aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuchukua nafasi ya Peter Ulanga ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Mbali na mabadiliko aliyoyafanya kwa Tanesco Rais Samia ameigusa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kumemteua aliyekuwa Katibu Mkuu, Said Othman Yakubu kuwa Balozi huku nafasi yake ikichukuliwa na Gerson Msigwa ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.

"Nafasi iliyoachwa wazi ya Mkurugenzi wa Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali itatangazwa baadae," ilieleza taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zuhura Yunus.

Kadhalika Rais Samia Amemteua, Dk Erasmus Kipesha kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi (TEA).


Makatibu Tawala wa Mikoa

Rais, ametengua uteuzi wa Abdallah Mohamed Malela, Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara. Badala yake amemteua Bahati Ibrahim Geuzye kuchukua nafasi hiyo. Kabla ya uteuzi huo, Bahati alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Pia amemteua Mohamed Gombati kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Geita. Kabla ya uteuzi huo, Gombati alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Maofisa Waandamizi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


Wakuu wa Wilaya

Ametengua uteuzi wa Hanafi Msabaha, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini na badala yake amemteua Mwanahamisi Mkunda kuchukua nafasi hiyo. Kabla ya uteuzi huo Mkunda aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke.

Pia amemteua Dk Stephen Mwakajumilo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Mariam Chaurembo atapangiwa kazi nyingine.


Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri

Amemteua Hassan Bakari Nyange kuwa Mkurugenzi (DED) wa Mtwara TC. Kabla ya uteuzi huu, Nyange alikuwa DAS Wilaya ya Namtumbo. Aidha, aliyekuwa Mkurugenzi (DED) wa Wilaya ya Mtwara TC, Kanali Emmanuel Mwaigobeko atapangiwa kazi nyingine.

Ametengua uteuzi wa Tatu Said Issike, Mkurugenzi wa Mtwara DC na kumteua Abeid Kafunda kuwa Mkurugenzi (DED) wa Mtwara DC. Kabla ya uteuzi huo, Kafunda alikuwa Mwanasheria katika Ofisi ya mkemia Mkuu wa Serikali.

Kadhalika amemteua, Reuben Jichabu kuwa Mkurugenzi (DED) wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Erica Yegella atapangiwa kazi nyingine.


Katibu tawala wa Wilaya

Rais Samia amemteua Francis Mgoloka kuwa Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Namtumbo. Kabla ya uteuzi huo Mgoloka alikuwa Katibu Tarafa Mswaki - Kilindi Handeni.

Aidha kwa mujibu wa taarifa ya uteuzi huo imesema kuwa Katibu Mkuu na Makatibu Tawala wa Mikoa wataapishwa Jumanne, Septemba 26, 2023 saa sita mchana Ikulu jijini Dar es Salaam.