Rais Samia ailetea neema sarafu ya bitcoin

Samia: Mwanza kuwa kitovu cha biashara EAC

Muktasari:

  • Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan ya jana Juni 13, 2021  kuhusu sarafu za mtandaoni imeipa fursa sarafu ya Bitcoin baada ya kutoa habari njema kwa soko hilo.

Dar es Salaam. Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan ya jana Juni 13, 2021 kuhusu sarafu za mtandaoni imeipa fursa sarafu ya Bitcoin baada ya kutoa habari njema kwa soko hilo.

Hotuba yake huko Mwanza ilifuata baada ya nchi ya El Salvador kutangaza kupitisha Bitcoin kama njia halali ya malipo ya zabuni sambamba na mataifa mengine ya Amerika Kusini na Kati kuonyesha utayari wao wa kutumia sarafu hiyo.

Akizungumza jijini Mwanza, Rais Samia Suluhu Hassan aliitaka Benki Kuu (BoT) kujitayarisha kwa matumizi ya sarafu mtandaoni, akisema wakati wa sarafu mtandaoni umefika, hivyo, ni muhimu kuanza maandalizi kuruhusu mabadiliko hayo.

Rais Samia alisema Benki kuu ya Tanzania inapaswa kuanza maandalizi muhimu ya mabadiliko ya hatua katika mtazamo wa ulimwengu juu ya benki, ikichagua sarafu za mtandaoni kama mustakabali wa fedha.

“Tumeshuhudia kuibuka kwa safari mpya kupitia mtandao.Najua kuwa mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania hawajakubali au kuanza kutumia njia hizi. Lakini wito wangu kwa Benki Kuu ni kwamba mnatakiwa kuanza kufanyia kazi maendeleo hayo. Benki Kuu inapaswa kuwa tayari kwa mabadiliko na sio kukutwa hamjajiandaa,” amesema.

Mbali na El Salvador na nchi chache za jirani, hii ni mara ya kwanza kwa Rais wa nchi yoyote duniani kukubali waziwazi matumizi ya sarafu za mtandaoni au njia ya ugatuzi ya benki.

Kauli hiyo ya Rais Samia imekuja sambamba na maoni ya hivi karibuni kutoka kwa Elon Musk ambaye amekuwa mshawishi mkubwa wa bei ya Bitcoin tangu kuanzishwa kwake zaidi ya mwongo mmoja uliopita.

Hivi karibuni, kiongozi huyo wa Tesla amesema kampuni yake ya magari ya umeme itakubali Bitcoin kama njia ya malipo.

Lakini mjasiriamali mwenye umri wa miaka 49 alilaumiwa na makala ya Coin Telegraph ambayo ilimnukuu Magda Wierzycka, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya huduma za kifedha ya Sygnia akisema mwenzake wa Afrika Kusini angeweza kuchunguzwa na mamlaka kwa ujanja wa soko.