Rais Samia aitisha kikao cha dharura usiku, atoa agizo

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameitisha kikao cha dharura Jumapili Mei 8 2022 usiku Ikulu ya Dar es Salaam kujadili tatizo la kupanda kwa bei ya mafuta nchini.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza mawazi, makatibu wakuu wa baadhi ya Wizara kutafuta suluhisho la haraka la kukabiliana na tatizo la kupanda bei ya mafuta nchini.

Mkuu huyo wa nchi ametoa agizo hilo baada ya kuitisha kikao cha dharura kilichofanyika usiku wa kuamkia leo Mei 9, 2022 Ikulu ya Dar es Salaam cha kujadili tatizo la kupanda kwa bei ya mafuta ya ptroli, dizeli na mafuta ya taa nchini.

Miongoni mwa waliohudhuria katika kikao hicho ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Nishati January Makamba, Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, makatibu wakuu wa wizara hizo na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) Alphayo Kidata.

Rais Samia ameitisha kikao hicho ikiwa zimepita siku tatu tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa naye alipoitisha kikao na baadhi ya mawaziri kufanya tathmini ya bei ya mafuta na kuangalia namna gani Serikali inaweza kufanya ili kupunguza athari ya bei ya mafuta na kuleta unafuu wa gharama za maisha kwa Watanzania.

Katika kikao chake Waziri Mkuu kilichofanyika usiku wa kuamkia leo Alhamisi Mei 5, 2022 jijini Dar es Salaam, Majaliwa alisema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Kikao hicho ambacho nacho kilifanyika usiku kiliwahusisha baadhi ya mawaziri wakiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati, January Makamba, Makatibu Wakuu, pamoja na watendaji wakuu wa taasisi za EWURA, TPDC na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).


Alhamisi ya wiki iliyopita sakata hilo la kupanda kwa bei ya mafuta liliingia bungeni baada Mbunge wa Kilindi (CCM), Omary Kigua kutoa hoja ya kutaka bunge liahirishe shughuli zake na kujadili tatizo hilo, hoja ambayo iliridhiwa na wabunge kupata nafasi ya kuijadili huku baadhi wakiishauri Serikali kuondoa tozo walizoweka katika mafuta angalau kwa Sh400 hadi Sh500 kwa miezi mitatu ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo.

Waziri wa Nishati, January Makamba akichangia hoja hiyo alisema Serikali iko tayari kufanya chochote ili kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini.

“Tumekubaliana hivi karibuni tutakuja na majawabu kuhusiana na suala hili,”alisema Makamba.

Baada ya mjadaala huo, Dk Tulia Ackson aliiagiza Serikali kupeleka bungeni hatua za muda mfupi itakazochukua kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Dk Tulia alisema alimuuagiza Waziri Makamba kupeleka kauli ya Serikali bungeni kesho Jumanne.

“Kauli ya mambo hayo waliyoyajadili na hatua mbalimbali ambazo Serikali itazichukua kwenye jambo hili. Kwasababu ni jambo la dharura na lazima tulifanye kwa udharura,” alisema Dk Tulia.

Aprili 30 mwaka huu Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) ilitangaza nauli mpya za mabasi ya mijini maarufu daladala na mabasi ya masafa marefu ambazo zitaanza kutumika Mei 14.

Bei hizo mpya za petroli, dizeli na mafuta ya taa ambazo zilianza kutumika Jumatano ya wiki iliyopota huku bei ya nishati hiyo ikizidi kupanda na kufikia zaidi ya Sh3, 000 kwa lita.

Akitangaza kiwango hicho kipya cha nauli Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe alisema mabasi ya mjini kuanzia Kilomita 0 hadi 10 nauli itakuwa Sh500 badala ya 400 na nauli ya Sh450 itakuwa ni 550.

"Kwa kilomita 30 nauli itakuwa 850 badala ya 750 na kwa kiliometa 35 nauli itakuwa 1000 na kwa huku kwa upande wa Kilometa 40 nauli itakuwa 1100" alisema Ngewe

Alisema kwa mabasi ya mkoani daraja la kawaida kwa kwa Kilometa 1 imeongezeka kwa asilimia 11 kutoka Sh 36 kwa kilometa moja hadi Sh41.

"Kwa daraja la kati imeongezeka kwa asilimia 6 abiria mmoja atalipa Sh56.88 kwa kilometa kutoka Sh53" alisema.

Hata hivyo, bei hizo mpya za nishati hiyo zilizua tafrani kwa baadhi ya wasafirishaji ambao katika baadi ya mikoa madereva wa mabasi madogo maarufu daladala waligoma kutoa huduma.

Madereva hao waligoma Alhamisi Mei 5 kutoa huduma wakitaka kuanza kutumika nauli mpya zilizotangazwa na Latra ambazo zingetakiwa kuanza Mei 14 mwaka huu.

Miongoni mwa maeneo ambayo madereva hao walifanya mgomo ni pamoja na Mkoa wa Arusha na Tanga.

Katika Jiji la Arusha mgomo huo uliodumu kuanzia asubuhi hadi jioni, ulisitishwa baada ya mamlaka kuridhia watoa huduma hao kuanza kutumia nauli mpya kabla ya muda.