Serikali yasema iko tayari kufanya chochote kupunguza bei ya mafuta

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Serikali iko tayari kufanya chochote ili kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini.

Dodoma. Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Serikali iko tayari kufanya chochote ili kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini.

Serikali yasema iko tayari kufanya chochote kupunguza bei ya mafuta

Akichangia hoja iliyotolewa na Mbunge wa Kilindi (CCM), Omary Kigua ya kupanda kwa bei ya mafuta leo Mei 5,2022, Makamba amesema jana Serikali ilikaa kutazama hatua za kuchukua za haraka za kukabiliana na changamoto hiyo.

Amesema hatua za kikodi zinataka mashauriano, ufuatiliaji wa sheria na kanuni zinaongoza uwekaji na uondoaji wa hizo tozo.

Amesema ushauri uliotolewa na wabunge wa kuondoa kodi wamelichukua lakini suala hilo linataka uzingatiaji wa sheria na kanuni zake na taratibu za nchi zinazohusiana na masuala ya kodi.

“Tumekubaliana hivi karibuni tutakuja na majawabu kuhusiana na suala hili,”amesema Makamba.

Ametaja hatua nyingine waliyochukua ni kutafuta namna mbadala ya kupata watu wa kuagiza mafuta kwa bei nafuu limetokana kama wabunge walivyoshauri.

Makamba amesema wamepokea maombi mengi, wamechakata na kwamba waliopita katika mchakato huo watazungumza nao katika mazungumzo ya wazi ili kuona kama wanaweza kupata mafuta kwa bei nafuu.

“Serikali iko tayari kufanya chochote kitakachowahakikishia bei nafuu ya mafuta. Pamoja na hatua za haraka ambazo ni za kikodi, Serikali imechukua hatua za kati,”amesema.

Amezitaja hatua hizo ni kuanzisha hifadhi ya Taifa ya kimkakati ya mafuta na kuanzisha mfuko wa kuhimili bei za mafuta ambao upo katika hatua za mwisho za kuandika andiko la baraza la mawaziri ambalo watapeleka katika kikao kijacho cha baraza la mawaziri ili mfuko huo uanze.

Amesema hatua nyingine ya kati ni kwa kushirikiana na sekta binafsi kuanzisha kituo kikubwa cha biashara ya mafuta yatakayotosheleza mahitaji ya muda mrefu.

Pia, amesema ameongea na mawaziri wenzake katika ukanda Afrika Mashariki, Zambia na Malawi kukutana katika mkutano wa dharura jijini Arusha lengo likiwa ni kujadiliana kama wanaweza kuunganisha nguvu na kujenga soko moja la ukanda huu.

Amesema kuwa na soko moja la ukanda litawezesha kuwa na mkono mmoja wenye nguvu wa kuweza kuamua namna ambavyo wataweza kutambua (ku-detect) bei ya mafuta.